Maelfu waandamana kupinga ziara ya Trump nchini Ireland
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141430-maelfu_waandamana_kupinga_ziara_ya_trump_nchini_ireland
Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika mitaa ya Dublin kupinga ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, nchini Ireland, huku wanaharakati wakilaani sera zake katika masuala ya kigeni, mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji, na masuala ya kijamii.
(last modified 2026-09-13T11:26:30+00:00 )
Sep 13, 2026 11:24 UTC
  • Maandamano dhidi ya Trump nchini Ireland
    Maandamano dhidi ya Trump nchini Ireland

Maelfu ya waandamanaji wamejitokeza katika mitaa ya Dublin kupinga ziara ya Rais wa Marekani, Donald Trump, nchini Ireland, huku wanaharakati wakilaani sera zake katika masuala ya kigeni, mabadiliko ya tabianchi, uhamiaji, na masuala ya kijamii.

Maandamano hayo yalihusisha mchanganyiko mpana wa vyama vya siasa, makundi ya wanaharakati, vyama vya wafanyakazi, na watu binafsi. Waandaaji walisema takriban watu 25,000 walihudhuria.

Waandamanaji walibeba mabango na bendera za Palestina, wakipaza sauti kulaani sera za kigeni za Trump, msimamo wake kuhusu Gaza, kukataa kwake kuwepo kwa sera za kulinda mazingira, ubaguzi wa rangi, pamoja na matumizi ya Uwanja wa Ndege wa Shannon na vikosi vya kijeshi vya Marekani.

Wakiandamana kutoka Garden of Remembrance kuelekea jengo la Dáil (Bunge la Ireland), waandamanaji waliokuwa na hasira  pia walimlaani vikali Trump kwa kuanzisha vita dhidi ya Iran.

Holly Eustance, mmoja wa waandamanaji, amenukuliwa akisema kuwa sera za Trump zinatishia viumbe hatarini na sayari nzima, akisema vita na mabadiliko ya tabianchi vinasababisha uharibifu mkubwa huku mifumo ya kisiasa na kiuchumi ikipendelea mabilionea badala ya watu wa kawaida.

Kundi la ‘Anti-Imperialist Action’ (Kundi la Kupinga Ubeberu) lilichoma bendera ya Marekani karibu na Mtaa wa Molesworth, likifyatua fataki na kupaza sauti kupinga uwepo wa wanajeshi wa Marekani katika uwanja wa ndege wa Shannon.

Wakiwa nje jengo la Dáil (Bunge la Ireland) waandamanaji walikosoa jinsi serikali ya Ireland ilivyoshughulikia ziara ya Trump. Mbunge wa chama cha Labour, Ciarán Ahern, aliwatuhumu maafisa wa serikali kwa “kujipendekeza,” huku Seneta Alice Mary Higgins akielezea ziara hiyo kama “tamthilia ya kuchukiza.”

Awali, Trump alionekana kupuuzia maswali kuhusu maandamano hayo, akidai kuwa huenda yalikuwa ya “kirafiki,” lakini waandamanaji walisisitiza kuwa ujumbe wao ulikuwa wazi: kwamba hakukaribishwa nchini Ireland.

Rais Donald Trump aliwasili Juamosi kwa ziara ya siku mbili nchini Ireland. Ziara hiyo imefanyika huku kukiwa na mojawapo ya operesheni kubwa zaidi za kiusalama kuwahi kutekelezwa na jeshi la polisi la Ireland (An Garda Síochána).