Libya yakamata dawa za kulevya za picha ya Gaddafi zilizoingizwa kutokea Ulaya
Libya imekamata shehena ya maelfu ya vidonge vya dawa za kulevya aina ya ecstasy, vilivyowekwa alama ya picha ya kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.
Kwa mujibu wa maafisa wa usalama, vidonge hivyo vilisafirishwa kwa njia ya magendo kutoka Ulaya.
Picha zilizotolewa na chombo cha usalama mjini Tripoli zimeonyesha magunia yenye vidonge vya rangi ya kahawia, vilivyotengenezwa kwa umbo la kichwa na mabega ya Gaddafi.
Vidonge hivyo vina michoro inayoakisi sura yake ya kipekee pamoja na vazi alilokuwa akilitumia.
Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa mwezi Januari mwaka huu, Libya imekuwa kitovu cha usafirishaji wa madawa ya kulevya ya kutengenezwa viwandani na aina nyinyingine za mihadarati, ambayo husafirishwa kwenda kwa watumiaji wa ndani na maeneo mengine ya Afrika Kaskazini pamoja na sehemu mbalimbali za bara la Afrika.
Ripoti hiyo, iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) ilisema, magenge ya biashara ya madawa ya kulevya yamekuwa yakitumia fursa ya hali ya machafuko nchini humo tangu mwaka 2011.
Kwa mujibu wa ripoti, maafisa wa usalama walipata taarifa kwamba genge moja lilikuwa likipanga kusafirisha dawa hizo kwa njia ya bahari.
Maafisa waliizuia shehena hiyo baada ya kuwasili na kugundua kwamba vidonge hivyo vilikuwa vimefichwa ndani ya gari la kubebea mizigo, taarifa hiyo iliongeza.
"Operesheni hiyo ilifanikisha kukamatwa vidonge vipatavyo 100,000 vya 'XTC' (Ecstasy)," ilifafanua taarifa hiyo na kuongeza kwamba idadi ya watuhumiwa kadhaa imewasilishwa kwa waendesha mashtaka…/