Bei za kukodisha Meli za Mafuta zapaa mara nane
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141458-bei_za_kukodisha_meli_za_mafuta_zapaa_mara_nane
Wakati Marekani ikidai kuwa na udhibiti kamili wa Lango-Bahari wa Hormuz, gharama za kukodisha meli za mafuta katika njia hiyo muhimu mno ya baharini zinaendelea kupaa na kuvunja rekodi.
(last modified 2026-09-14T10:57:10+00:00 )
Sep 14, 2026 10:54 UTC
  • Bei za kukodisha Meli za Mafuta zapaa mara nane

Wakati Marekani ikidai kuwa na udhibiti kamili wa Lango-Bahari wa Hormuz, gharama za kukodisha meli za mafuta katika njia hiyo muhimu mno ya baharini zinaendelea kupaa na kuvunja rekodi.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, wastani wa mapato ya meli kubwa sana za mafuta (supertankers) umeongezeka kwa zaidi ya asilimia 40 tangu mwanzoni mwa mwezi wa Septemba.

Hata hivyo, kupanda bei za kukodisha meli hizo hakutokani tu na mgogoro katika Lango-Bahari wa Hormuz.

Gazeti la Financial Times hivi karibuni liliripoti kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani, lilitaja gharama kubwa za kutoa ulinzi wa anga na limeomba meli zinazopitia hapo zipitishe mizigo yao ndani ya vipindi maalumu na kwa saa maalumu.

Matokeo yake ni kwamba, gharama ya kukodisha meli ya mafuta kwa ajili ya safari kutoka Ghuba ya Uajemi hadi China imefikia kiwango cha juu kabisa kuwahi kurekodiwa, ikizidi dola 800,000 kwa siku.

Wakati huo huo, sambamba na kupungua shughuli za usafirishaji kupitia Lango-Bahari La Hormuz na kuongezeka mahitaji ya vyanzo mbadala barani Asia, gharama za usafirishaji wa meli kutoka Ghuba ya Mexico hadi Asia nazo zimefikia viwango visivyotasawirika. Gharama ya safari moja katika njia hiyo imezidi dola milioni 29 — kiwango kinacholingana na takriban dola 15 kwa kila pipa la mafuta.

Hii ina maana kwamba katika bei yote inayolipwa kwa pipa moja la mafuta, dola 15 hutumika tu kwa ajili ya kulisafirisha pipa hilo hadi mahali linapokwenda.

Hayo yamekuja huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran akitangaza kuwa kufunguliwa upya Lango-Bahari la Hormuz kunategemea Marekani kurejea na kuheshimu ahadi zake chini ya Maelewano wa Islamabad na si vinginevyo.