Rais wa Iran: Tunahitaji mageuzi ya kweli katika mifumo ya kimataifa
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa suala la utawala na mamlaka shirikishi ya dunia na kuimarishwa mfumo wa pande nyingi lina umuhimu mkubwa zaidi hivi sasa.
Dakta Masoud Pezeshian amesema hayo jana katika kikao cha faragha cha viongozi wa nchi wanachama wa Kundi la BRICS kilichofanyika mjini New Delhi, India na kubainisha kwamba, endapo Mkataba wa Umoja wa Mataifa utashindwa kuwalinda watu dhidi ya matumizi haramu ya nguvu, na endapo sheria za kimataifa zitakuwa za lazima kwa baadhi ya nchi huku kwa wengine zikitafsiriwa kwa matakwa yao, basi hatuwezi kuzungumzia mfumo wa kweli wa pande nyingi katika utawala wa dunia.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, uhalali wa mfumo wowote wa utawala hupimwa kwa uwezo wake wa kulinda haki za nchi zote, ziwe ndogo au kubwa.
Kadhalika amesema katika hotuba yake kwenye mkuutano huo kwamba, uchokozi na uvamizi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran ulisababisha vifo vya watu wasio na hatia na kuharibu miundombinu muhimu ya nchi, pamoja na miundombinu ya kiuchumi na ya kiraia.
Aidha amesema, Marekani na utawala huo unaokalia ardhi za Palestina, katika siku ya kwanza pekee ya vita hivyo vilivyodumu kwa siku 40, walimuua shahidi Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na watoto 168 wasio na hatia katika shule ya Minab.
Rais wa Iran ameongeza kuwa, shambulio dhidi ya shule ya Minab na uwanja wa michezo wa Lamerd lilidhihirisha wazi sera ya upande mmoja, uchochezi wa vita na ukatili wa Marekani na utawala ghasibu unaokalia kwa mabavu ardhi za Palestina, sambamba na jinsi kutotekeleza majukumuu yake Umoja wa Mataifa na Baraza lake la Usalama, vinavyoweza kutishia moja kwa moja maisha ya binadamu.
Amesema pia kwamba, matukio ya miaka ya hivi karibuni yameonyesha kwamba usalama endelevu hauwezi tena kujengwa kwa misingi ya kuwepo usalama kwa baadhi ya nchi huku nyingine zikiwa katika hali ya ukosefu wa usalama.
Usalama endelevu hupatikana pale ambapo mamlaka na uhuru wa nchi vinaheshimiwa, na hakuna nchi inayoweza kutumia ardhi yake kama msingi wa kutishia au kushambulia nchi nyingine.