Guinea-Bissau yaendesha kura ya maoni ya kumuongezea Rais mamlaka
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141086-guinea_bissau_yaendesha_kura_ya_maoni_ya_kumuongezea_rais_mamlaka
Wapiga kura Guinea-Bissau nchi inayoongozwa na jeshi walipiga kura jana Jumapili walishiriki katika kura ya maoni ya kumuongezea Rais mamlaka zaidi kabla ya uchaguzi mkuu unaolenga kurejesha utawala wa kiraia baadaye mwaka huu.
(last modified 2026-08-31T04:33:49+00:00 )
Aug 31, 2026 04:31 UTC
  • Guinea Bissau yaendesha kura ya maoni
    Guinea Bissau yaendesha kura ya maoni

Wapiga kura Guinea-Bissau nchi inayoongozwa na jeshi walipiga kura jana Jumapili walishiriki katika kura ya maoni ya kumuongezea Rais mamlaka zaidi kabla ya uchaguzi mkuu unaolenga kurejesha utawala wa kiraia baadaye mwaka huu.

Usalama uliimarishwa katika maeneo ya kimkakati katikamji mkuu Bissau huku askari wa ulinzi wa taifa na polisi wakipangwa katika maeneo muhimu.

Zoezi la kupiga kura katika kura ya maoni lilifungwa jana jioni huku matokeo ya awali yakitarajiwa kuanza kutangaza kesho Jumanne.

Kura ya maoni huko Guinea-Bissau imefanyika jana Jumapili ikiwa ni chini ya miezi 10 baada ya kujiri mapinduzi ambapo jeshi lilichukua madaraka katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika inayozungumza lugha ya Kireno.

Mmiliki wa duka, Halimatou Traore aliliambia shirika la habari la AFP kuwa anatumai katiba mpya italeta mabadiliko chanya huko Guinea- Bissau.

"Misukosuko mfululizo ambayo nchi imepitia imeathiri vibaya sana mapato yangu. Mambo yakienda vizuri, Guinea-Bissau itaingia katika njia mpya," alisikika akisema Halimatou Traore wakati akisubiri kupiga kura jana Jumapili.

Baraza la kijeshi la Guinea- Bisaau linasema kuwa mabadiliko hayo yanalenga kuleta utulivu katika taasisi mbalimbali kabla ya uchaguzi mpya wa urais na bunge uliopangwa kufanyika tarehe 6 Desemba kwa lengo la kurejesha madaraka ya uongozi wa nchi kwa raia.