Rais wa Iran aihimiza BRICS kulinda kanuni ya kutotumia mabavu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141432-rais_wa_iran_aihimiza_brics_kulinda_kanuni_ya_kutotumia_mabavu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt. Masoud Pezeshkian, ametoa wito kwa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS kuchukua jukumu “lenye ufanisi zaidi” katika kulinda mamlaka ya kitaifa na kusimamia kanuni ya kimataifa ya kutotumia nguvu, hasa katika kipindi hiki cha sasa chenye changamoto nyingi.
(last modified 2026-09-14T04:03:40+00:00 )
Sep 13, 2026 11:29 UTC
  • Rais Pezeshkian wa Iran akihutubia mkutano wa 18 wa viongozi wa BRICS jijini New Delhi, India, Septemba 12, 2026. (Picha na president.ir)
    Rais Pezeshkian wa Iran akihutubia mkutano wa 18 wa viongozi wa BRICS jijini New Delhi, India, Septemba 12, 2026. (Picha na president.ir)

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Dkt. Masoud Pezeshkian, ametoa wito kwa kundi la mataifa yanayoinukia kiuchumi la BRICS kuchukua jukumu “lenye ufanisi zaidi” katika kulinda mamlaka ya kitaifa na kusimamia kanuni ya kimataifa ya kutotumia nguvu, hasa katika kipindi hiki cha sasa chenye changamoto nyingi.

Rais Pezeshkian ameyasema hayo Jumapili katika hotuba yake kwenye Mkutano wa 18 wa Viongozi wa BRICS, unaofanyika katika mji mkuu wa India, New Delhi, chini ya kaulimbiu: “Kujenga kwa Ajili ya Ustahimilivu, Ubunifu, Ushirikiano na Uendelevu.”

Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa matukio ya hivi karibuni katika eneo la Asia Magharibi, hasa hujuma za vita vya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran, yamebainisha wazi kuwa madhara ya kulenga miundombinu ya kiuchumi, nishati, na maendeleo ya nchi, yanaweza ndani ya muda mfupi kuvuka mipaka na kuwa na athari za kieneo na kimataifa.

Ameongeza kuwa: “Wananchi wa Iran wamelipa gharama kubwa kwa vitendo hivi vya uchokozi. Wanawake, wanaume, watoto, na raia wasio na hatia wamepoteza maisha, huku miundombinu iliyojengwa kwa miongo kadhaa ili kuendeleza maendeleo ya nchi ikiharibiwa. Matukio haya ni ukumbusho wa wajibu mzito wa jamii ya kimataifa kulinda raia na kuzuia hali ya kuhalalisha mashambulizi dhidi ya maeneo ya kiraia.”

Aidha amesema: "Wananchi wa Gaza na Lebanon wanaendelea kukabiliwa na athari za jinai na mauaji ya kimbari. Haiwezekani kuzungumzia sheria za kimataifa bila kuwepo na mwitikio madhubuti wa kimataifa dhidi ya uchokozi wa kijeshi, mauaji ya binadamu, na uharibifu wa maisha yao. Hivyo, BRICS inapaswa pia kuchukua nafasi yenye ufanisi zaidi katika kutetea mamlaka ya kitaifa, ukamilifu wa ardhi, na kuzingatia kanuni ya kutotumia nguvu.”

Wakati huohuo, Rais Masoud Pezeshkian amekanusha vikali madai ya uwongo kwamba Iran inatafuta silaha za nyuklia. Amesisitiza kuwa Iran imekuwa ikifanya kazi kila mara ndani ya mfumo wa sheria za kimataifa, na ingekuwa haijajiunga na Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia (NPT) iwapo ingekuwa na nia ya kutafuta silaha hizo.

Akizungumza na chombo cha habari cha India Today pembezoni mwa mkutano huo wa BRICS, Rais Pezeshkian amesema kuwa shughuli za nyuklia za Iran zimekuwa chini ya uangalizi na ukaguzi wa kina wa kimataifa.

Kuhusu uhusiano wa kieneo, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa Iran ina uhusiano wa kirafiki na nchi jirani, ikiwemo Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Saudi Arabia, Pakistan, na Qatar, pamoja na Russia na China. Ametaja kambi za kijeshi za Marekani katika eneo kuwa chanzo kikuu cha matatizo na mivutano.

Ikumbukwe kuwa BRICS, ambayo awali iliundwa na Brazil, Russia, India, China, na Afrika Kusini, ilipanuka mwaka 2024 na kuingiza Misri, Ethiopia, Iran, UAE, na Saudi Arabia, huku Indonesia ikijiunga mwaka 2025. Aidha, nchi kama Belarus, Bolivia, Kazakhstan, Cuba, Malaysia, Nigeria, Thailand, Uganda, Uzbekistan, na Vietnam zimekuwa nchi washirika wa kundi hilo tangu mwaka jana.

Kwa sasa, kundi hili linawakilisha asilimia 45 ya idadi ya watu duniani na linazalisha zaidi ya asilimia 35 ya Pato la Taifa la dunia (GDP) kwa vipimo vya uwezo wa kununua