Vita vya Marekani vyadhoofisha mno Uchumi wa Imarati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141456-vita_vya_marekani_vyadhoofisha_mno_uchumi_wa_imarati
Takwimu rasmi zilizotolewa na Muungano wa Falme za Kiarabu zinaonesha kuwa, vita vilivyochochewa na Marekani na utawala wa Kizayuni katika ukanda huu vimefuta karibu nusu ya mapato ya sekta ya utalii ya Imarati (UAE).
(last modified 2026-09-14T10:54:22+00:00 )
Sep 14, 2026 10:53 UTC
  • Vita vya Marekani vyadhoofisha mno Uchumi wa Imarati

Takwimu rasmi zilizotolewa na Muungano wa Falme za Kiarabu zinaonesha kuwa, vita vilivyochochewa na Marekani na utawala wa Kizayuni katika ukanda huu vimefuta karibu nusu ya mapato ya sekta ya utalii ya Imarati (UAE).

Televisheni ya Al-Mayadeen imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, takwimu rasmi kutoka Idara ya Uchumi na Utalii ya Dubai zinaonesha kushuka kwa kiasi kikubwa idadi ya watalii wa kigeni wanaotembelea Imarati katika miezi minane ya kwanza ya mwaka 2026 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.

Takwimu za hivi karibuni za idara hiyo zinaonesha kuwa Dubai ilipokea watalii wa kigeni milioni 6.97 kati ya Januari na Agosti 2026, huku idadi hiyo ikiwa milioni 12.54 katika kipindi kama hicho mwaka 2025.

Matokeo yake ni kwamba, idadi ya watalii wanaoingia Dubai imepungua kwa takriban watalii milioni 5.57, ikiwa na maana ya kushuka kwa takriban asilimia 44.4 katika miezi minane ya kwanza ya mwaka 2026 ikilinganishwa na mwaka 2025.

Takwimu hizo zinazohusiana na utendaji wa sekta ya utalii ya Muungano wa Falme za Kiarabu zilitolewa kabla ya maonyesho ya kila mwaka ya "Arabian Travel Market" huko Dubai. Hilo ni tukio ambalo makampuni ya utalii hukutana kila mwaka ili kufufua sekta hiyo.

Matokeo haya yanakuja baada ya mwaka ulioweka rekodi kwa utalii wa Dubai yaani mwaka 2005 ambapo idadi ya wageni waliotembelea Muungano wa Falme za Kiarabu ilifikia takriban milioni 19.6. Hata hivyo, vita dhidi ya Iran vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni unaozikalia kwa mabavu ardhi za Palestina vimesababisha hasara kubwa kwa sekta ya utalii ya Imarati.

Na huko Marekani pia, wananchi wa nchi hiyo wakiwemo wakulima wanalalamikia ugumu wa maisha na kupaa bei za mafuta, huku shirika la GasBuddy la Marekani ambalo linafuatilia bei za mafuta nchini humo likisema kuwa, hivi sasa kila galoni moja la mafuta ya dizeli linauzwa kwa dola 9.999 katika jimbo la California.