Je, Muqawama wa Yemen Ulishindaje Mkakati wa Saudi Arabia?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141452-je_muqawama_wa_yemen_ulishindaje_mkakati_wa_saudi_arabia
Kufuatia matukio ya hivi karibuni nchini Yemen, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa ikisisitiza kuwa kutatuliwa matatizo ya Yemen hakuwezekani kupitia kuendelezwa mzingiro na utunishaji misuli ya kijeshi.
(last modified 2026-09-14T09:29:08+00:00 )
Sep 14, 2026 09:27 UTC
  • Je, Muqawama wa Yemen Ulishindaje Mkakati wa Saudi Arabia?

Kufuatia matukio ya hivi karibuni nchini Yemen, Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa taarifa ikisisitiza kuwa kutatuliwa matatizo ya Yemen hakuwezekani kupitia kuendelezwa mzingiro na utunishaji misuli ya kijeshi.

Msimamo huu unakuja huku matukio ya hivi karibuni katika pwani ya Magharibi ya Yemen yakiweka wazi tena kushindwa kwa mkakati wa kijeshi wa kutaka kuidhibiti nchi hiyo, na kubadilisha uwiano wa nguvu katika mojawapo ya maeneo muhimu zaidi ya kimkakati Asia Magharibi. Matukio ya sasa nchini Yemen hayawezi kutazamwa bila kuzingatia zaidi ya muongo mmoja wa vita, mzingiro na uingiliaji wa kigeni. Mnamo mwaka 2015, huku ikitegemea nguvu zake za kijeshi na ikiungwa mkono kisiasa, kijeshi na kiintelijensia na Marekani, Saudi Arabia iliamini kuwa ingeweza kubadilisha haraka uwiano wa kisiasa huko Yemen. Hesabu hiyo ilifeli ambapo muungano huo wa kijeshi haukuweza kuvunja azma ya watu wa Yemen, wala kuunda mfumo imara wa kisiasa unaokubalika kwa Saudi Arabia au kujihakikishia usalama wa kudumu. Leo, baada ya zaidi ya muongo mmoja, vita vilevile vya kichokozi vilivyokusudiwa kudhibiti nguvu ya Ansarullah vimegeuza kundi hilo kuwa moja ya nguvu muhimu zaidi zinazoathiri usalama wa eneo.

Hatua za karibuni za kusonga mbele Wahouthi kando kando ya pwani ya magharibi ya Yemen zimefanya kufeli kwa mkakati huu kuonekana wazi zaidi. Kufika kwao katika maeneo muhimu ya pwani na udhibiti wa Lango-Bahari la Bab al-Mandab ni jambo linalovuka mipaka ya mafanikio ya uwanja wa vita pekee, ambapo hali hii inabadilisha ramani ya usambazaji wa nguvu. Kundi ambalo huko nyuma lilijulikana zaidi kutokana na mivutano ya ndani ya Yemen, sasa linadhibiti mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini duniani. Eneo hili ni njia muhimu sana ya kupitia meli za biashara na inaunganisha mabara ya Asia na Ulaya. Hivyo, matukio yanayojiri katika pwani ya magharibi ya Yemen yana uhusiano wa moja kwa moja na usalama wa usafirishaji wa baharini, biashara ya kimataifa na usafirishaji wa nishati.

Katika muktadha huu, hatua iliyochukuliwa na Riyadh pia ni muhimu kuzingatiwa. Ombi la Saudi Arabia la kutaka kuongezewa msaada kutoka Marekani ili kukabiliana na kusonga mbele kwa wapiganaji wa Houthi linaonyesha waziwazi hali ya kukwama kwa mkakati wa nchi hiyo ya kifalme. Licha ya kumiliki mojawapo ya majeshi yenye gharama kubwa zaidi katika eneo, Saudi Arabia ilijiingiza katika vita vya Yemen na kujikuta, miaka kadhaa baadaye, ikiendelea kutegemea Washington kwa ajili ya usalama wake dhidi ya wapiganaji ambao walitarajiwa kushindwa haraka na bila matatizo makubwa. Hali hii ya mgongano ndiyo inapaswa kuzingatiwa katika uchambuzi wowote kuhusu vita vya Yemen. Ni wazi kuwa nguvu za kijeshi zinazonunuliwa kutoka nje huwa hazileti moja kwa moja nguvu za kisiasa. Kauli ya mtafiti wa Saudi Arabia, Fuad Ibrahim, pia ina umuhimu katika muktadha huu. Hahusishi kushindwa kwa vikosi vinavyoungwa mkono na muungano wa Saudia na usaliti au biashara ya askari pekee, bali anasisitiza juu ya ushujaa wa wapiganaji wa Yemen. Hali hii inafichua udhaifu wa kimsingi katika mkakati wa Saudi Arabia. Vita hivyo vilianzishwa kwa kutegemea fedha, silaha na vikosi vya niaba, lakini katika uwanja wa vita, vikakabiliwa na ari ya kweli na utashi wa kisiasa. Taifa linalochukulia vita kuwa hatua ya kulinda mamlaka na ardhi yake haliwezi kushindwa kwa kutumia nguvu ya kijeshi pekee.

Marekani nayo haiwezi kujivua majukumu katika mlingano huo. Katika kipindi chote cha vita, Washington ilitoa taarifa za kijasusi, silaha na uungaji mkono wa kisiasa kwa muungano wa Saudi Arabia, lakini sasa inakabiliwa na matokeo yanayokinzana kabisa na malengo ya awali ya uingiliaji huo. Marekani ilitaka kuimarisha mfumo wa usalama inaoupendelea katika eneo, lakini kiuhalisia, vita vya Yemen vimevuruga nguzo nyingine ya mfumo huo.

Hivyo, hali halisi ya sasa ni kwamba vita vya Yemen vimefichua wazi udhaifu na mipaka ya nguvu ya Saudi Arabia badala ya kuonyesha uwezo wake, na kuangazia gharama za kutegemea Washington kwa ajili ya kudhamini usalama, badala ya kuimarisha uingiliaji wa Marekani katika eneo.

Kwa mtazamo huu, taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran inatoa ujumbe unaovuka wito wa kupunguza mvutano katika eneo. Iran inasisitiza kuwa mgogoro wa Yemen hauwezi kutatuliwa kwa kuigeuza nchi hiyo kuwa uwanja wa ushindani wa kijeshi kati ya mataifa ya kigeni. Usalama wa Bahari ya Shamu hauwezi kudhaminiwa kwa kuondoa upande mmoja wa milingano ya nguvu na kulazimisha mipango ya usalama kutoka nje. Suluhisho pekee linapatikana katika kurejea kwenye meza ya mazungumzo, kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya Yemen kuondoa mzingiro, na kutambua haki za watu wa nchi hiyo.