China: Tuko tayari kutetea kwa nguvu haki za Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema kuwa uhusiano na ushirikiano wa nchi yake na Iran ni wa kimkakati na kwamba Beijing inatangaza rasmi kwamba iko tayari kuimarisha mazungumzo na ushirikiano na Iran, na kutetea kwa dhati haki na maslahi halali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Shirika la habari la TASS limemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, akisisitizia umuhimu wa uhusiano wa kimkakati kati ya nchi yake na Tehran wakati alipokutana na Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran mjini Beijing leo Jumatano.
Wang Yi amesema: "China na Iran zina ushirikiano wa kina wa kimkakati. China pia iko tayari kuimarisha mazungumzo na ushirikiano na Tehran na kutetea kwa dhati haki na maslahi halali ya Iran."
Akionesha umuhimu wa nafasi ya Iran katika siasa za kigeni za Beijing, Waziri wa Mambo ya Nje wa China ameitaja Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni mshirika muhimu wa kimkakati.
Kabla ya hapo, Wang Yi alikutana na kufanya mashauriano na Araghchi pembezoni mwa mkutano wa BRICS uliofanyika nchini India Jumamosi na Jumapili iliyopita.
Kauli hizo zimetolewa wakati wa ziara ya Abbas Araghchi mjini Beijing na kukutana kwake na Wang Yi. Katika mkutano huo, pande hizo mbili zimejadiliana uhusiano wa nchi mbili na njia za kuimarisha ushirikiano huo.
Katika taarifa yake kuhusu mkutano huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa China amesema: "Hatutaki kuona mivutano ya kikanda inaongezeka wala hatutaki mivutano hiyo ifike hadi Yemen na Bahari Nyekundu."
Ameongeza kuwa: "Tunatoa mwito kwa Washington na Tehran kufanya mashauriano ya kina kuhusu masuala ambayo bado hayajatatuliwa na kujenga upya mfumo wa mazungumzo kwa kuzingatia makubaliano yaliyofikiwa kwenye mapatano ya Islamabad."