Je, Mpango wa "Kuifanya Yemen kama Syria" Ulifeli Vipi?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141518-je_mpango_wa_kuifanya_yemen_kama_syria_ulifeli_vipi
Vyanzo vya habari mjini Sana'a, mji mkuu wa Yemen, vimeripoti kuhusu njama kubwa ya kuifanya Yemen ikabiliwe na hali ya machafuko kama ile ya Syria, mpango ambao hatimaye umefeli licha ya kushirikishwa makundi ya kitakfiri yanayohusishwa na utawala wa muda wa Al-Julani.
(last modified 2026-09-17T05:49:27+00:00 )
Sep 17, 2026 05:45 UTC
  • Je, Mpango wa

Vyanzo vya habari mjini Sana'a, mji mkuu wa Yemen, vimeripoti kuhusu njama kubwa ya kuifanya Yemen ikabiliwe na hali ya machafuko kama ile ya Syria, mpango ambao hatimaye umefeli licha ya kushirikishwa makundi ya kitakfiri yanayohusishwa na utawala wa muda wa Al-Julani.

Likinukuu vyanzo vya habari mjini Sana'a, gazeti la Lebanon la Al-Akhbar limeripoti kuwa Vita vya Pwani ya Magharibi, ambavyo vilimalizika kwa kushindwa vikosi vinavyoungwa mkono na Riyadh, vilikwamisha mpango wa Saudi Arabia wa kutaka kurudia "hali ya mporomoko kama ilivyotokea Syria" nchini Yemen; mpango ambao ulihusisha kuhamishwa vikosi vya watu wenye misimamo mikali kutoka Syria kuja Yemen kupitia ardhi ya Saudi Arabia. Chombo hicho cha habari cha Lebanon kimenukuu vyanzo vya Yemen vikieleza kuwa Saudi Arabia imekuwa ikifanyia kazi mpango huu kwa zaidi ya mwaka mmoja. Katika muktadha huu, Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani wa Iraq, Baqir Jabr al-Zubeidi, amefichua katika mahojiano ya karibuni na vyombo vya habari vya Iraq kwamba, kufuatia kufeli kwa operesheni za kijeshi za nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi dhidi ya Ansarullah, daraja la anga lilianzishwa ili kusafirisha magaidi kutoka Syria kwenda Yemen.

Swali linabakia kuwa je, njama hii dhidi ya Yemen ilifeli vipi?

Hoja ya kwanza ni kwamba, tofauti na vikosi vya jeshi la Syria, vikosi vya Yemen vilikuwa na utayari na mafunzo muhimu ya kukabiliana na njama hii hatari. Utayari huo uliwezesha vikosi vya Yemen si tu kupenya katika safu za adui bali pia kusonga mbele kwa kasi kuelekea kusini na kutoa pigo kubwa dhidi ya maadui hao. Likinukuu vyanzo vya kuaminika na kusisitiza ubora wa Ansarullah katika mafunzo na mbinu za kijeshi, gazeti la Al-Akhbar limeripoti kuwa kundi hilo lilikuwa limejiandaa kwa vita hivi kwa takriban mwaka mmoja. Miezi kadhaa kabla, lilifanikiwa kupenya katika safu za makundi yenye silaha yanayoungwa mkono na Riyadh, jambo lililoliwezesha kufanya mashambulizi ya awali dhidi ya maghala ya silaha na vituo vilivyojengwa na Saudi Arabia kwa miaka mingi ili kujiandaa kwa ajili ya operesheni kubwa magharibi na mashariki mwa Yemen.

Hoja nyingine ni kwamba wapinzani wa Ansarullah ya Yemen si tu hawana utayari wa kijeshi na mshikamano unaohitajika kwa ajili ya mapambano, bali pia wanakabiliwa na migawanyiko mikubwa na ya wazi ya ndani pamoja na ukosefu wa uongozi wenye umoja. Aidha, sehemu kubwa ya vikosi hivi inaundwa na mamluki kutoka nchi nyingine na ambao hawana motisha ya kitaifa wala kidini ya kukabiliana na vitisho, tofauti kabisa na vikosi vya Ansarullah ambavyo vinapigana kwa ari kubwa ya kitaifa na kidini kwa ajili ya kulinda umoja wa ardhi ya nchi yao.

Pia ni muhimu kuzingatia kuwa vikosi vya Yemen vinajaribu kuvunja mzingiro uliowekwa dhidi ya nchi hiyo na Saudi Arabia, mzingiro ulioanza kutekelezwa mwaka 2015 na ambao bado unaendelea hadi leo. Hivyo, vikosi vya Yemen, ambavyo sasa vimejiandaa vizuri zaidi kuliko huko nyuma, vimechukua hatua za kuvunja mzingiro huo na kuzuia mipango ya kuigeuza Yemen kuwa kama Syria, huku vikipata mafanikio makubwa katika kuvunja njama za adui na katika madeni ya vita.