Rais wa Sudan Kusini avunja serikali yake kuelekea uchaguzi mkuu
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141678-rais_wa_sudan_kusini_avunja_serikali_yake_kuelekea_uchaguzi_mkuu
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametoa amri ya kuvunjwa serikali na kuundwa serikali ya mpito. Hatua hiyo imechukuliwa miezi mitatu kabla ya kufanyika uchaguzi wa kwanza katika historia ya nchi hiyo baadaye mwaka huu.
(last modified 2026-09-24T03:30:42+00:00 )
Sep 24, 2026 03:28 UTC
  • Rais wa Sudan Kusini avunja serikali yake kuelekea uchaguzi mkuu

Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametoa amri ya kuvunjwa serikali na kuundwa serikali ya mpito. Hatua hiyo imechukuliwa miezi mitatu kabla ya kufanyika uchaguzi wa kwanza katika historia ya nchi hiyo baadaye mwaka huu.

Muda wa uongozi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, iliyoundwa chini ya makubaliano ya amani ya mwaka 2018 yaliyomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe, ulimalizika usiku wa kuamkia Jumatano.

Kwa mujibu wa amri hiyo, manaibu wote wa rais, mawaziri na wakurugenzi wameondolewa madarakani, huku Bunge la Taifa na mabunge ya majimbo pia yakivunjwa. Hata hivyo, Salva Kiir ataendelea kuongoza vikosi vya jeshi na kusimamia mfumo wa mahakama.

Kwa mujibu wa amri hiyo pia, rais wa sasa anaweza kuendelea kuwa rais wa muda wakati wa kipindi cha uchaguzi, hadi rais atakayechaguliwa atakapoanza rasmi majukumu yake.

Uchaguzi wa Sudan Kusini, ambao umeahirishwa mara mbili, umepangwa kufanyika Disemba mwaka huu, licha ya serikali kushindwa kutekeleza vipengele vingi muhimu vya makubaliano ya amani.

Wakati huohuo, zoezi la uandikishaji wapiga kura bado halijakamilika, vikosi vya kijeshi bado havijaunganishwa kuwa jeshi moja lililoungana, na katiba mpya iliyokuwa ikisubiriwa bado haijakamilishwa.

Siku chache zilizopita Rais Salva Kiir alitia saini mabadiliko ya sheria yanayoondoa masharti ya kukamilisha katiba ya kudumu na sensa kabla ya uchaguzi wa Desemba, hatua ambayo imelalamikiwa vikali na muungano mkuu wa upinzani nchini humo.

Mabadiliko hayo yanalenga kufungua njia ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 22 mwaka huu. Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu Sudan Kusini ilipopata uhuru mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan.

Muungano wa Upinzani wa Sudan Kusini, ambao ulitia saini makubaliano ya amani ya mwaka 2018, umeyakataa mabadiliko hayo. Umesema yamefanywa bila mashauriano ya kutosha baina ya pande zilizotia saini makubaliano hayo.

Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.