Araghchi: Uingiliaji wa kijeshi hauwezi kuleta usalama; kutumia mabavu hakuwezi kuleta amani
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi amesema kuwa uingiliaji wa kijeshi hauwezi kuleta usalama, wala matumizi ya mabavu hayawezi kuleta amani. Araghchi amesisitiza haja ya kufanyika mabadiliko ya msingi kutoka katika sera za kijeshi na uingiliaji wa masuala ya nchi nyingine, kuelekea maendeleo endelevu, kuheshimu mamlaka ya kitaifa ya nchi, na kuimarisha amani ya kudumu.
Akizungumza katika mkutano wenye kaulimbiu “Wito wa Kubadili Mwelekeo wa Dunia: Kuweka Maendeleo Katikati, Kurejesha Ubinadamu na Haki katika Dunia Inayozidi Kuwa ya Kichaa”, uliofanyika katika Global Town Hall 2026 na kuandaliwa na Jumuiya ya Sera za Kigeni ya Indonesia siku ya Jumamosi, Araghchi amesema kuwa miongo kadhaa ya uingiliaji wa kigeni, shinikizo la kijeshi na vita visivyo na mwisho katika eneo la Asia Magharibi, imedhihirisha kwamba uingiliaji wa kijeshi hauleti usalama na matumizi ya mabavu hayawezi kuleta amani.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa janga la Gaza na uhalifu unaoendelea kufanywa na utawala wa Israel ni miongoni mwa mifano iliyo wazi na ya kutisha zaidi ya mfumo huu ambao umeshindwa.
Ameonya kuwa, kumeibuka mwenendo hatari ambapo nguvu za kijeshi hazitumiki tena kama hatua ya mwisho, bali zimegeuka kuwa nyenzo ya kudumu ya kubadilisha hali ya kisiasa na kiusalama katika eneo.
Amesema katika mazingira kama hayo, uchokozi unaanza kuzoeleka, ongezeko la mivutano linawekwa katika mifumo ya kudumu, na uharibifu unageuka kutoka kuwa matokeo ya vita na kuwa chombo cha kufanikisha malengo ya kisiasa.
Araghchi ameelezea operesheni za kijeshi za Marekani na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Iran kuwa sehemu ya mwenendo huo mpana, akizitaja kuwa kinyume cha sheria, zisizo za haki na za uchokozi, huku akibainisha kuwa zilifanyika bila uchokozi wa awali.
Aidha, amezungumzia kampeni za mauaji yaliyolenga maafisa wa Iran, vitisho dhidi ya viongozi wa kisiasa, ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya nchi, pamoja na kutoadhibiwa kwa vitendo vya uchokozi. Amesema kushindwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya vitendo hivyo kutasababisha, hatua kwa hatua, kudhoofika kwa mipaka na kanuni zilizowekwa na sheria za kimataifa.