Pakistan: Makubaliano yetu na Saudia hayatoathiri uhusiano wetu na Iran
Msemaji wa Jeshi la Pakistan amesema kuwa makubaliano ya kijeshi ya nchi yake na Saudi Arabia pamoja na Uturuki maarufu kwa jina la Makubaliano ya Makka, hayatoathiri uhusiano wa Tehran na Islamabad.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Ahmed Sharif Chaudhry, amesema hayo na kuongeza kuwa, makubaliano ya kijeshi baina ya Pakistan, Saudi Arabia na Uturuki — yanayojulikana kama "Makubaliano ya Makka" — yana lengo la kujilinda tu na hayatarajiwi kuathiri uhusiano na Iran.
Chaudhry ameiambia tovuti ya "Al Arabiya English" kuwa makubaliano hayo yamebuniwa kama ngao ya pamoja ya kujilinda yenye lengo la kuleta amani, utulivu na usalama katika eneo hili lote na hayalengi kufanya uchokozi au kushambulia nchi nyingine. Pia amesisitiza kuwa kama ambavyo makubaliano hayo hayatafanya uhusiano wa Pakistan na Iran kuwa mgumu ni vivyo hivyo hayatoathiri uhusiano wa kimkakati wa nchi yake na China.
Akijibu swali kuhusu hatua ambayo Pakistan itachukua iwapo nchi mwanachama itashambuliwa, msemaji huyo wa Jeshi la Pakistan amesema kuwa hakuna nchi au jeshi linalotangaza hadharani maelezo ya operesheni zake za kijeshi au namna mahususi ambayo majukumu yake ya ulinzi yanatekelezwa.
Vilevile amesema: Makubaliano ya Makka hayajitambulishi kwa jina la Muungano wa Kiislamu au wa Waislamu, wala hayana kipengele chochote kinachozuia kushiriki nchi zisizo za Kiislamu.
Ameongeza kuwa lengo la makubaliano hayo ni kuimarisha utulivu, amani na usalama wa kikanda, jambo ambalo linahusisha nchi zote si za Kiislamu tu.
Kuhusu hali ya mambo nchini Afghanistan, msemaji wa jeshi la Pakistan amesema kuwa, Islamabad haikusudii kuingilia masuala ya Afghanistan; hata hivyo, amedai kuwa Afghanistan chini ya utawala wa Taliban inatumiwa kama jukwaa la kuajiri, kutoa mafunzo na kuratibu mashambulizi ya kigaidi.