Misri yasema Bwawa la GERD la Ethiopia limejengwa “kinyume cha sheria”
Misri inasisitiza kuwa Bwawa la GERD la Ethiopia limejengwa “kinyume cha sheria” na inahifadhi haki yake ya kuchukua hatua zozote inazoziona kuwa muhimu kulinda usalama wake wa maji.
Haya yamesemwa na Waziri wa Umwagiliaji na Rasilimali za Maji wa Misri, Hani Sewilam. Ameyasema hayo wakati wa mkutano jijini Cairo na wawakilishi wa vyombo vya habari vya kigeni nchini Misri.
Misri na Ethiopia zimekuwa katika mvutano kwa miaka mingi kuhusu Bwawa la GERD linalojulikana pia kama Al-Nahda, ambalo Addis Ababa ilianza kulijenga kwenye Mto Nile wa Buluu mnamo 2011.
Sewilam amesema kukamilika kwa bwawa hilo na kupita kwa muda hakumaanishi kuwa Misri imekubali hali hiyo au kuachana na haki zake.
Amesema Azimio la Kanuni za 2015 lililotiwa saini na Misri, Ethiopia, na Sudan lilikusudiwa kuwa mwongozo wa kuweka ahadi za ushirikiano, kufikia makubaliano kuhusu ujazaji wa awali wa bwawa hilo na uendeshaji wa kila mwaka, pamoja na uratibu na kubadilishana taarifa.
Sewilam amesema azimio hilo haliipei Ethiopia haki ya kuchukua hatua za upande mmoja kuhusu bwawa hilo, na kuongeza kuwa Misri inachukulia mwendelezo wa ujazaji na uendeshaji bila makubaliano kama ukiukaji wa ahadi hizo.
Amesema, “Bwawa hili ni kinyume cha sheria. Misri ina haki ya kuchukua hatua mwafaka ili kuondoa madhara yanayosababishwa kwake.”
Sewilam ameonya kuwa uendeshaji wa bwawa hilo bila uratibu unaweza kusababisha ongezeko la ghafla au kupungua kwa kasi kwa mtiririko wa maji, jambo linaloweza kuathiri mabwawa katika nchi za Misri na Sudan.
Pia amekanusha madai ya Ethiopia kwamba Misri inapokea “sehemu kubwa zaidi” ya maji ya Mto Nile.
Amesema mgao wa kila mwaka wa Misri wa bilioni 55.5 za mita za ujazo unawakilisha takriban 2.7% ya karibu trilioni 2 za mita za ujazo za mvua zinazonyesha katika Bonde la Mto Nile.
Sewilam amesema Ethiopia ina zaidi ya hekta milioni 18 za ardhi ya kilimo ikilinganishwa na takriban hekta milioni 4.03 za Misri.
Misri na Sudan zimetoa wito wa kuwepo kwa makubaliano ya kisheria ya pande tatu kati ya Misri, Sudan, na Ethiopia kuhusu ujazaji na uendeshaji wa GERD ili kuhakikisha haki zao za maji na maslahi yao hayadhuriki.
Hata hivyo, Ethiopia inasema kuwa uendeshaji wa bwawa hilo hauhitaji makubaliano na Sudan au Misri na inasisitiza kuwa haina nia ya kudhuru maslahi ya nchi nyingine.