Moto warindima katika Kitovu cha Usafirishaji Mafuta Saudi Arabia
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141440-moto_warindima_katika_kitovu_cha_usafirishaji_mafuta_saudi_arabia
Vyombo mbalimbali vya habari jana Jumapili vilisambaza picha zinazoonesha moshi mzito ukifuka kutoka kwenye kituo cha mafuta vya Yanbu katika pwani ya Bahari ya Shamu. Taarifa zinasema kuwa, kituo hicho ndicho kilichokuwa kinaisaidia Marekani kupakia mafuta baada ya Iran kufunga Lango-Bahari la Hormuz.
(last modified 2026-09-14T11:15:43+00:00 )
Sep 14, 2026 07:35 UTC
  • Moto warindima katika Kitovu cha Usafirishaji Mafuta Saudi Arabia

Vyombo mbalimbali vya habari jana Jumapili vilisambaza picha zinazoonesha moshi mzito ukifuka kutoka kwenye kituo cha mafuta vya Yanbu katika pwani ya Bahari ya Shamu. Taarifa zinasema kuwa, kituo hicho ndicho kilichokuwa kinaisaidia Marekani kupakia mafuta baada ya Iran kufunga Lango-Bahari la Hormuz.

Vyombo hivyo vya habari vimesema kuwa shughuli za kupakia mafuta katika kituo hicho cha Yanbu kwenye pwani ya Bahari Nyekundu zilisimama mchana wa Jumapili huku ripoti kutoka duru za kuaminika zikionesha kuwa shughuli za kupakia mafuta katika kituo hicho muhimu cha kimkakati zimesimama kikamilifu na hazikusimama kwa siku moja tu.

Picha za vyombo hivyo vya habari zinaonesha wingu zito la moshi likifuka kutoka eneo hilo baada ya jeshi la Yemen kukipiga kituo hicho jana Jumapili. Vyombo hivyo vimesema kuwa, shughuli za kupakia mafuta katika kituo hicho zilikuwa tayari zimesimama kabisa tangu siku tatu kabla ya hapo.

Picha za satelaiti zinaonesha wingu kubwa la moshi likienea kwa takriban kilomita 80 kando ya Bomba la Mafuta la Mashariki-Magharibi, huku moto ukionekana ukiwaka katika maeneo sita tofauti kando ya kituo hicho. Data za satelaiti ya NASA pia zimerekodi moto mkubwa ukiwaka katika moja ya vituo vilivyounganishwa na bomba hilo la kusafirishia mafuta yakiwemo yaendayo Marekani.

Bomba la Mafuta la Mashariki-Magharibi la Saudi Arabia (Petroline) lilishambuliwa Alkhamisi iliyopita, jambo lililosababisha kusimamishwa shughuli zake zote kama hatua ya tahadhari.

Bomba hilo lenye urefu wa kilomita 1,200 husafirisha mafuta ghafi kutoka eneo la Abqaiq pwani ya Ghuba ya Uajemi hadi bandari ya Yanbu kwenye Bahari ya Shamu, likiwa na uwezo wa kusafirisha hadi mapipa milioni 7 kwa siku.

Umuhimu wa kimkakati wa bomba hili uliongezeka sana katika miezi ya hivi karibuni. Baada ya Marekani kuivamia kijeshi Iran na baada ya Tehran kuamua kulifunga Lango Bahari la Hormuz, Saudi Arabia iliamua kubadilisha njia ya kusafirisha mafuta na kuyapelekea kwa njia ya nchi kavu hadi kwenye kituo cha Yanbu na hatimaye kusafirisha mafuta hayo nje ya eneo hili kwa kutumia Bahari ya Shamu. Makadirio yanaonesha kuwa mapipa milioni 4 hadi 5 ya mafuta — sawa na asilimia 4–5 ya usambazaji wote wa mafuta duniani — yalikuwa yakipita katika njia hiyo kila siku.