Wachimba migodi haramu wasiopungua 14 wamepoteza maisha mgodini Afrika Kusini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140588-wachimba_migodi_haramu_wasiopungua_14_wamepoteza_maisha_mgodini_afrika_kusini
Polisi ya Afrika Kusini leo imetangaza kuwa wachimbaji wadogo wa madini wasiopungua 14 wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa katika mgodi ambao hautumiki nchini humo.
(last modified 2026-08-11T11:25:05+00:00 )
Aug 11, 2026 11:22 UTC
  • Wachimba migodi haramu wasiopungua 14 wapoteza maisha Afrika Kusini
    Wachimba migodi haramu wasiopungua 14 wapoteza maisha Afrika Kusini

Polisi ya Afrika Kusini leo imetangaza kuwa wachimbaji wadogo wa madini wasiopungua 14 wamefariki dunia na wengine wengi kujeruhiwa katika mgodi ambao hautumiki nchini humo.

Jeshi la Polisi ya Afrika Kusini limeripoti kuwa wachimbaji hao walikutwa wameaga dunia katika mgodi mmoja karibu na mji wa Rustenburg, takriban kilomita 130 kaskazini-magharibi mwa mji wa Johannesburg.

Jeshi la Polisi la Afrika Kusini hata hivyo halikutoa maelezo zaidi kuhusu mazingira ya vifo hivyo, lakini limeeleza kuwa Kamishna wa Polisi wa mkoa alikuwa njiani kuelekea mgodini.

Afrika Kusini ina makumi ya maelfu ya wachimbaji wadogo wa madini wanaofanya kazi kinyume cha sheria katika migodi ya dhahabu na platinamu ambayo haitumiwi tena na makampuni ya uchimbaji. Wachimbaji hao wasio rasmi huingia migodini kutafuta mabaki ya madini ili kuyauza. Mara nyingi hufanya kazi bila vifaa sahihi vya usalama na wakati mwingine husalia chini ya ardhi kwa wiki kadhaa.

Rustenburg ni kitovu cha uchimbaji wa platinamu nchini Afrika Kusini, nchi ambayo ina akiba kubwa zaidi ya platinamu duniani.

Mamlaka husika za Afrika Kusini zinasema kuwa shughuli zisizo rasmi za uchimbaji madini ni tatizo kubwa nchini humo na zinahusishwa na magenge ya uhalifu.

 Wachimbaji hao wasio rasmi wanajulikana sana kwa jina la "zama zamas," neno linaloweza kutafsiriwa kama "watu wanaojaribu bahati yao."