Kwa nini Marekani inakanusha vita ilivyoanzisha yenyewe?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141268-kwa_nini_marekani_inakanusha_vita_ilivyoanzisha_yenyewe
Katikati ya mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya Marekani na Iran, White House inaendelea kukwepa kutumia neno "vita," kuhusu mgogoro uliopo na badala yake kutumia ibara za "operesheni za kijeshi" na "hatua chache"; hata hivyo, hali halisi ya mambo, kuanzia mashambulizi ya makombora na vifo au majeruhi hadi kutumwa katika eneo idadi kubwa ya askari na meli za kivita za Marekani, inaonyesha taswira tofauti kabisa.
(last modified 2026-09-07T06:11:19+00:00 )
Sep 07, 2026 06:07 UTC
  • Kwa nini Marekani inakanusha vita ilivyoanzisha yenyewe?

Katikati ya mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya Marekani na Iran, White House inaendelea kukwepa kutumia neno "vita," kuhusu mgogoro uliopo na badala yake kutumia ibara za "operesheni za kijeshi" na "hatua chache"; hata hivyo, hali halisi ya mambo, kuanzia mashambulizi ya makombora na vifo au majeruhi hadi kutumwa katika eneo idadi kubwa ya askari na meli za kivita za Marekani, inaonyesha taswira tofauti kabisa.

Msimamo huu umekuwa changamoto kubwa kwa simulizi rasmi ya Washington hivi karibuni ambapo utawala wa Trump unajitahidi kuepuka kutumia neno "vita" hata wakati makombora yanarushwa, wanajeshi na raia wakiuawa au kujeruhiwa na Lango-Bahari la Hormuz likiwa katika hali ya mvutano.

Kuna suala zito zaidi nyuma ya mchezo huu wa maneno: White House inataka kukwepa uwajibikaji wa kisiasa kwa vita ilivyoanzisha yenyewe kupitia shambulio la kijeshi dhidi ya Iran. Awamu hii ya vita ilianza tarehe 28 Februari kwa mashambulizi dhidi ya Iran yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni, yakifuatiwa na mfululizo wa mashambulizi ya kulipizana kisasi kati ya Tehran na Washington. Kwa hivyo, simulizi ya tukio hili haiwezi kuwasilishwa kana kwamba Marekani iliingilia kati kwa ajili tu ya kukabiliana na mgogoro uliokuwepo, bali chanzo halisi cha awamu hii ya vita ulikuwa uamuzi mbovu wa Washington na Tel Aviv kuanzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Iran.

Ni katika muktadha huu ndipo jaribio la kuepuka neno "vita" linapopata uzito wa kisiasa. Ikulu ya Marekani inafahamu vizuri kwamba kukiri kuhusika na kuanzisha vita kunaibua maswali magumu. Kwa nini shambulio lilifanyika? Lengo lake lilikuwa nini? Kwa nini operesheni iliyokusudiwa kuwa ya muda mfupi imechukua miezi kadhaa? Na kwa nini Marekani sasa, ikiwa na zaidi ya askari 50,000 na makumi ya meli za kivita katika eneo, imekwama katika mgogoro ambao mwisho wake hauonekani wazi? Na zaidi ya yote, kwa nini walipa kodi na wapiga kura wa Marekani wabebe gharama za uamuzi ambao serikali iliahidi ungekuwa wa muda mfupi na wenye wigo mdogo tu?

JD Vance, Makamu wa Rais wa Marekani, anasema: "Siitii hali hii kuwa vita." Pamoja na hayo, hali halisi ya mambo haibadiliki kutokana na kauli hiyo. Marekani imeishambulia Iran, Iran imejibu mashambulizi, uhasama umeanza upya na sasa Washington imetuma vikosi vikubwa vya majini na askari ili kudumisha mashinikizo ya kijeshi na kiuchumi dhidi ya Iran. Hii si "doria" ya kawaida au operesheni ya kipolisi tena; ni vita vilivyoanzishwa na Washington, ambavyo sasa inajaribu kupunguza uzito wa dhima yake ya kisiasa kwa kuvipa jina jingine. Migongano ya kauli za watawala wa Marekani inazidi kuangazia suala hili. Wakati Vance akiepuka kutumia neno "vita," Trump anazungumzia ushindi, huku akielezea mgogoro huo kuwa "mdogo" katika kauli zake za hivi karibuni. Hii ni licha ya ripoti za karibuni kuonyesha kuwa wanajeshi 18 wa Marekani wameuawa katika vita hivyo na gharama kwa Marekani imezidi dola bilioni 37.5.

Hivyo, suala hili si la uchaguzi wa maneno tu. Ikulu ya Marekani inataka kudai ushindi katika vita huku ikijitenga na majukumu ya kuanzisha vita hivyo na kubeba gharama zake. Ikiwa mgogoro huu kwa hakika ni "mafanikio ya kijeshi," kwa nini usitajwe kwa jina lake halisi? Na ikiwa hivi si vita, kwa nini serikali ya Marekani imetuma makumi ya maelfu ya askari na meli za kivita, na kutumia mabilioni ya dola kwa mashambulizi ya anga na mzingiro wa majini? Jaribio la kupunguza uzito wa mgogoro huu linapata umuhimu wa kipekee kadiri uchaguzi wa katikati ya muhula unavyokaribia nchini Marekani. Uchokozi dhidi ya Iran sasa umekuwa suala la ndani kwa utawala wa Trump; kupanda kwa bei ya mafuta na shinikizo la mfumuko wa bei, pamoja na kupungua kwa uungwaji mkono wa umma, kunaweza kuongeza gharama ya kisiasa ya vita hivyo kwa Chama cha Republican. Katika utafiti wa hivi karibuni uliofanywa na Reuters/Ipsos, ni asilimia 25 tu ya Wamarekani wameeleza kuwa vita hivi vina thamani ya gharama ambazo Marekani inazilipa.

Washington inaweza kubadilisha jina la vita hivi, lakini haiwezi kubadilisha ukweli kuhusu namna vilivyoanza. Marekani ndiyo iliyoanzisha vita, na sasa inajaribu kufuta mgogoro wenyewe kutoka kwenye rekodi rasmi kabla ya gharama za kisiasa kuwawajibisha wale waliofanya uamuzi huo wa kujitia kitanzi.