Vyombo vya kutunga sheria vya Libya vyasisitiza mchakato wa kisiasa ufuate Katiba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141374-vyombo_vya_kutunga_sheria_vya_libya_vyasisitiza_mchakato_wa_kisiasa_ufuate_katiba
Vyombo viwili vikuu vya nchini Libya yaani Baraza la Wawakilishi la Libya (HoR) na Baraza Kuu la Serikali (High Council of State) vimesisitiza kuwa mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo unapaswa kufanyika ndani ya mfumo wa Tamko la Katiba na Makubaliano ya Kisiasa yanayosimamia kazi za mabaraza hayo mawili.
(last modified 2026-09-11T09:24:19+00:00 )
Sep 11, 2026 09:20 UTC
  • Vyombo vya kutunga sheria vya Libya vyasisitiza mchakato wa kisiasa ufuate Katiba

Vyombo viwili vikuu vya nchini Libya yaani Baraza la Wawakilishi la Libya (HoR) na Baraza Kuu la Serikali (High Council of State) vimesisitiza kuwa mchakato wa kisiasa wa nchi hiyo unapaswa kufanyika ndani ya mfumo wa Tamko la Katiba na Makubaliano ya Kisiasa yanayosimamia kazi za mabaraza hayo mawili.

Taarifa hiyo imetolewa kufuatia mkutano kati ya Spika wa HoR, Aguila Saleh na Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Serikali, Mohamed Takala, uliofanyika chini ya usimamizi wa Uturuki.

Vyombo hivyo viwili vya kutunga sheria nchini Libya vimeonesha kuwa viko tayari kuandaa mkutano wa pamoja wa "Kamati ya 6+6" katika siku zijazo ili kuiwezesha kamati hiyo kukamilisha majukumu yake kuhusu sheria za uchaguzi.

"Kamati ya 6+6," iliyoundwa kwa pamoja na HoR na Baraza Kuu la Serikali, ilifikia makubaliano mwezi Juni 2023 kuhusu sheria za kusimamia uchaguzi wa rais na bunge. Baadaye, HoR ilifanyia marekebisho sheria hizo za uchaguzi mwezi Oktoba mwaka huo lakini Baraza Kuu la Serikali lilipinga baadhi ya marekebisho hayo. Hali hiyo ilisababisha kucheleweshwa utekelezaji wa sheria hizo na kukwama kazi za kamati hiyo huku kukiwa na mivutano kuhusu mamlaka moja ya utendaji pamoja na masharti na taratibu za kufanya uchaguzi.

Katika hatua iliyofuata, "Kamati ya 4+4" ilitia saini makubaliano ya mwisho tarehe 30 Agosti mwaka huo huo chini ya usimamizi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuisaidia Libya (UNSMIL). Shabaha ya makubaliano hayo ilikuwa ni kuweka mazingira mazuri ya kufanyika uchaguzi wa rais na bunge ndani ya kipindi kisichozidi miezi 24, chini ya mamlaka moja ya utendaji na taasisi za kitaifa.

Matokeo muhimu ya makubaliano hayo ni pamoja na kufanya marekebisho ya muundo wa bodi ya Tume Kuu ya Taifa ya Uchaguzi na kushughulikia masuala kadhaa ambayo hayajatatuliwa katika sheria za uchaguzi, hasa kuruhusu wanajeshi kugombea na kupiga kura katika uchaguzi wa rais, pamoja na kuruhusu watu wenye uraia wa nchi mbili kugombea, kwa sharti kwamba mshindi aachane na uraia wake usio wa Libya kabla ya kula kiapo cha katiba.