Je, vita vimezidisha vipi hali ya kutengwa kielimu utawala wa Kizayuni?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141346-je_vita_vimezidisha_vipi_hali_ya_kutengwa_kielimu_utawala_wa_kizayuni
Tovuti ya Kizayuni ya Calcalist imeripoti kuwa sehemu ya Israel katika ufadhili wa utafiti wenye itibari wa Ulaya imepungua kwa kiasi kikubwa, huku kukiwa na ongezeko la visa vya watafiti wa kigeni wanaokataa kushirikiana na taasisi za Israel.
(last modified 2026-09-10T05:52:46+00:00 )
Sep 10, 2026 05:50 UTC
  • Je, vita vimezidisha vipi hali ya kutengwa kielimu utawala wa Kizayuni?

Tovuti ya Kizayuni ya Calcalist imeripoti kuwa sehemu ya Israel katika ufadhili wa utafiti wenye itibari wa Ulaya imepungua kwa kiasi kikubwa, huku kukiwa na ongezeko la visa vya watafiti wa kigeni wanaokataa kushirikiana na taasisi za Israel.

Utawala wa Kizayuni umekuwa ukisisitiza mara kwa mara kuwa elimu na teknolojia ni vyanzo muhimu vya nguvu na alama kuu ya maendeleo yake. Hata hivyo, katika miaka ya hivi karibuni, vita na vikwazo vya kimataifa vimepunguza uhusiano na ushirikiano wa kitaaluma wa utawala huo na mataifa mbalimbali, hasa nchi za Ulaya, jambo linaloibua maonyo mengi kutoka kwa jamii ya wasomi wa Israel. Swali linalojitokeza ni je, vita vimepelekea vipi utawala huo kutengwa kielimu?

Jinai na unyama unaofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya raia huko Palestina, Lebanon, Syria, na Iran umezua hisia kali za chuki dhidi ya utawala huo miongoni mwa jamii ya kimataifa, zikiwemo duru za kitaaluma katika nchi mbalimbali. Vyombo vya habari vya Kizayuni, vikiashiria wasomi wa Israel, vimeripoti kupungua kwa utayari wa jamii ya wasomi katika nchi mbalimbali, zikiwemo zile za Ulaya, wa kushirikiana na wenzao wa Israel katika nyanja za kielimu.

Vyombo vya habari vya Israel vimebainisha kuwa wanafunzi na wahadhiri katika nchi mbalimbali wanaandamana kupinga sera za Israel za kuchochea vita na vitendo visivyo vya kibinadamu dhidi ya watu wasio na hatia. Watafiti kutoka nje wanaepuka kabisa kushirikiana na wenzao wa Israel, kwani wanaona kuwa gharama za kisiasa, zile zinazohusiana na vyombo vya habari, au za kimaadili zinazotokana na ushirikiano huo ni kubwa mno. Tovuti ya Kizayuni ya Calcalist inaripoti kuwa visa vilivyorekodiwa vya kukataa kushirikiana, au kuzuia ushirikiano, na Wazayuni katika nyanja za kielimu viliongezeka kutoka visa 20 mnamo Novemba 2025 hadi visa 50 mnamo Mei 2026. Ripoti ya mwaka 2026 ya Taasisi ya Samuel Neaman, yenye makao makuu yake Israel kwenyewe, inawasilisha taswira tata zaidi, ambapo inathibitisha kuongezeka kwa mashinikizo ya vikwazo na malalamiko ya vyuo vikuu huku ikitoa onyo kali kuhusu matokeo yake.

Hoja nyingine muhimu ni kwamba vita na hali ya kutokuwa na utulivu wa kijamii inayotokana navyo, vikijumuishwa na hatua ya wasomi wa nchi nyingine ya kukataa kushirikiana kielimu na Wazayuni, vimesababisha "kuondoka kwa wataalamu" na wakati huo huo kuongezeka kwa wimbi la uhamiaji wa kinyumenyume wa Wazayuni kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Israel. Kwa kweli, jambo linalowatia wasiwasi mkubwa watawala wa Israeli ni kuongezeka kwa kasi idadi ya watu wanaohama ardhi hizo na kurejea katika nchi walizotoka. Ripoti zinaonyesha kwamba sehemu kubwa ya watu hawa ni wataalamu walio na viwango vya juu vya masomo katika sekta ya teknolojia ya kisasa. Kuhama huku ambako mara nyingi hujulikana katika chambuzi za Wazayuni kama "kukimbia kwa bongo", kumezua hofu kubwa kuhusu matokeo ya muda mrefu kwa uwezo wa kiuchumi na kielimu wa Israel. Wakosoaji wa vita wanaonya kuhusu athari mbaya zinazoweza kusababishwa na hali hii ya kukimbia bongo kwa uchumi na mustakabali wa Israel. Wengine pia wanaonya kwamba ikiwa mwenendo huu utaendelea, motisha ya kuhama na kukimbia kutoka ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel itaongezeka taratibu. Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeandika kuwa taathira za kukimbia wataalamu wa kizayuni kutoka ardhi hizo huenda zisionekane katika takwimu za kiuchumi za sasa, lakini baada ya miaka mitano au kumi hivi, zitaonekana wazi zaidi katika ubora wa rasilimali watu, usajili wa hataza, mashirika ya teknolojia na uhamiaji wa matabaka ya wasomi katika utawala huo.