Kwa nini Marekani Inahusisha Mgogoro wa Yemen na Iran?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141418-kwa_nini_marekani_inahusisha_mgogoro_wa_yemen_na_iran
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa madai ya uongo ya Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, hayawezi kubadili uhalisia wa mambo kwamba Ansarallah ya Yemen ni kundi huru linalofanya maamuzi yake lenyewe, halipokei maagizo kutoka kwa mtu yeyote wala kufanya kazi kama kibaraka wa upande mwingine.
(last modified 2026-09-13T09:22:26+00:00 )
Sep 13, 2026 09:19 UTC
  • Kwa nini Marekani Inahusisha Mgogoro wa Yemen na Iran?

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesisitiza kuwa madai ya uongo ya Marco Rubio, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, hayawezi kubadili uhalisia wa mambo kwamba Ansarallah ya Yemen ni kundi huru linalofanya maamuzi yake lenyewe, halipokei maagizo kutoka kwa mtu yeyote wala kufanya kazi kama kibaraka wa upande mwingine.

Kauli hii ya Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, inalenga hasa suala ambalo Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anajaribu kulificha. Washington kwa mara nyingine tena inajaribu kuutenganisha mgogoro wa Yemen na muktadha wake halisi na kuidhihisha Iran, badala ya chanzo halisi, kama sababu kuu ya machafuko yanayoendelea katika eneo. Kwa kudai kuwa Ansarallah ni "kibaraka wa Iran" na kwamba Iran ndiyo inayochochea baadhi ya mashambulizi ya kundi hilo dhidi ya Saudi Arabia, kimsingi Rubio anajenga simulizi ya kisiasa inayokusudiwa kuondoa lawama kwa Marekani na kuhalalisha sera za nchi hiyo za kuingilia mambo ya eneo.

Uhusiano wa Iran na Ansarallah ni jambo linalojulikana wazi. Tehran hutoa uungaji mkono wa kisiasa na kimkakati kwa harakati ya muqawama ya Yemen, na uhusiano huo umeimarika zaidi kadiri miaka inavyosonga mbele. Pamoja na hayo, haiwezi kusemekana kuwa kutokana na hali hiyo, Ansarallah ni nguvu iliyo chini ya amri na udhibiti wa Tehran au kwamba kila operesheni yake ya kijeshi hufanywa kwa maelekezo ya Iran. Hata tafiti zilizofanywa na vituo vya utafiti vya Marekani yenyewe zinasisitiza kuwa Ansarallah ina uhuru wa kufanya maamuzi yake yenyewe. Hapa ndipo hasa hoja ya Rubio inapokosa mashiko. Inaepuka kwa makusudi kuweka tofauti kati ya "ushirikiano," "uungaji mkono" na "amri" ili iweze kuhusisha moja kwa moja kila hatua inayochukuliwa na Ansarullah na Iran.

Upotoshaji huu una lengo maalumu la kisiasa. Marekani inataka kuwasilisha kila mgogoro wa kikanda kama "tishio linalosababishwa na Iran na vibaraka wake" ili kuhalalisha uwepo wake wa kijeshi na uingiliaji wake wa mambo ya ndani ya eneo hili. Simulizi hii inapuuza wazi historia ya vita vya Yemen, vita vilivyoanza mwaka 2015 kwa uingiliaji wa kijeshi ulioongozwa na Saudi Arabia, ambapo Marekani ilitoa taarifa za kijasusi, silaha, na msaada wa kioperesheni kwa muungano huo. Washington haitaki mtu yeyote leo ahoji ni nchi zipi ziligeuza vita vya Yemen kuwa mgogoro wa muda mrefu wa kibinadamu na kiusalama; hivyo, inachagua njia rahisi zaidi ya kuituhumu Iran, ili kuficha nafasi na dhima yake yenyewe. Hata hivyo, hali halisi ya mambo haitoi nafasi ya kufanyika hadaa hiyo. Leo, Ansarullah ni nguvu kubwa nchini Yemen ambayo imeimarisha muundo wake wa kisiasa na kijeshi unaojitegemea, katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja wa vita. Uamuzi wa harakati hiyo wa kuikabili Saudi Arabia na vikosi washirika wake unatokana na tathmini yake yenyewe kuhusu usalama na mustakabali wa Yemen. Kuhusisha maamuzi hayo moja kwa moja na Tehran si uchambuzi, bali ni mbinu ya kisiasa ya kuhamisha lawama.

Kwa Iran, umuhimu wa simulizi hii unavuka mipaka ya mzozo wa maneno tu, ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani. Washington inadai kuwepo kwa "mkono wa Iran" katika mashambulizi ya Yemen wakati ambapo eneo hilo linapitia mojawapo ya vipindi vyake nyeti zaidi vya kiusalama. Lango-Bahari la Bab el-Mandeb, Bahari ya Shamu, Ghuba ya Uajemi, na Lango-Bahari la Hormuz vinafungamana, kwa maana kwamba tukio lolote la kijeshi katika eneo hili linaweza kuathiri usalama wa nishati na biashara duniani. Katika mazingira haya, kuhusisha operesheni za mhusika mmoja wa kikanda na Iran kunaweza kuunda msingi wa kisiasa unaohitajika ili kupanua wigo wa makabiliano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Lengo la Washington liko wazi kiasi kwamba halihitaji ufafanuzi wa kina: Kwanza, ni kujenga taswira ya kwamba "Iran iko nyuma ya kila mgogoro"; pili, kuhusisha vitendo vya wahusika wa kikanda na Tehran; na tatu, kutoa uhalali wa kisiasa wa kuwekwa mashinikizo au kuchukuliwa hatua za kijeshi dhidi ya Iran. Huu ni mtindo ambao umekuwa ukijirudia katika sera za Marekani kwa miaka mingi. Marekani huanza kwa kumtuhumu mdau wa kikanda kama nguvu inayotegemea Iran, kisha hutaja vitendo vyake kama "shambulio la Iran," na hatimaye kuwasilisha hatua yake ya kijeshi ya kulipiza kisasi kama kitendo halali cha kujilinda. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikanushi kuwa na uhusiano na Ansarullah, lakini haikubali kuwajibika kwa maamuzi huru ya harakati hiyo. Tofauti hii lazima iwekwe wazi. Kuunga mkono muqawama wa kikanda ni sera ya kimkakati; kukubali tuhuma ya "kuongoza operesheni" ni jambo tofauti kabisa. Washington haiwezi, kwa kuweka lebo tu, kupuuza uhuru wa kufanya maamuzi wa wadau wa kikanda au kuitwisha Tehran mzigo wa migogoro inayotokana na sera zao huru wenyewe. Kwa hivyo, jibu la Baghaei kwa Rubio kimsingi ni onyo kwamba Washington haiwezi kufuta historia yake ya uingiliaji, au kubadilisha uhalisia wa mambo na tuhuma zisizo na msingi, kwa kuhusisha kila mgogoro wa kikanda na Iran. Mgogoro wa Yemen haukusababishwa na Iran, bali ni matokeo ya mapambano na muqawama wa Wayemen dhidi ya uingiliaji wa kigeni na miaka mingi ya vita.