Iran yaiambia IAEA: Ukaguzi wa kawaida wa nyuklia ‘hauwezekani’ katikati ya uchokozi
-
Ofisi ya Mwakilishi wa Iran katika wakala wa IAEA
Iran imekataa matakwa ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) kwa ajili ya kurejelewa ukaguzi wa kawaida, ikisema kuwa kutarajia utekelezaji wa kawaida wa hatua za usalama huku Iran ikiendelea kukabiliwa na hujuma za kichokozi ni jambo "lisilo na mantiki" na "lisilowezekana kutekelezwa."
Katika taarifa ya kina iliyosambazwa kwa nchi wanachama wa IAEA siku ya Jumatano, Ofisi ya Mwakilisi wa Kudumu wa Iran katika wakala wa IAEA imepinga wito wa hivi karibuni wa Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo Rafael Grossi ambaye ametaka kuruhusiwa tena wakaguzi wao kufika katika maeneo ya nyuklia, akisema kuwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki unapuuza uhakika wa mambo katika eneo linalojiri mapigano.
Ofisi ya Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika wakala wa IAEA imeeleza kuwa wakala huo kuwa na matarajio kwamba utatekeleza kama kawaida shughuli za ufuatiliaji na udhibiti wa masuala ya usalama wa nyuklia (safeguards) huku ukifahamu vyema hali mbaya ya mambo ambayo ni natija ya vitisho na uchokozi endelevu dhidi ya Iran ni jambo lisilo na mantiki.
Hati hiyo ya tarifa ya kina iliyosambazwa jana kwa nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki imeeleza kuwa IAEA yenyewe imekiri kuhusu uwepo wa hatari hiyo ambapo hadi kufikia mwezi Juni mwaka jana ilikuwa wakala huo ulikuwa tayari umewaondoa wakaguzi wake wote nchini Iran kwa sababu za kiusalama.
Taarifa hiyo pia imeongeza kuwa, wakala wa IAEA ulikuwa umefichua bila sababu za msingi "taarifa nyeti sana kuhusu asili na mahali ilipo akiba ya nyuklia ya Iran" bila idhini ya awali.
Taarifa hiyo imeonya kuwa ufichuzi wa aina hiyo unaziweka taasisi hizo katika hatari kubwa, hasa wakati ambapo "maadui sugu wa Iran wanazisaka kwa udi na uvumba " shabaha kama hizo.