Oct 04, 2023 13:20 UTC
  • Iran: Wakaguzi wa IAEA wametimuliwa kutokana na mienendo ya uhasama

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amesema wakaguzi wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) waliofukuzwa hapa nchini wanatoka katika nchi tatu za Ulaya; na kwamba walitumuliwa kutokana na mienendo yao ya kiuhasama na misimamo ya kisiasa dhidi ya Tehran.

Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran alisema hayo jana Jumatano hapa Tehran pambizoni mwa mkutano wa Baraza la Mawaziri na kuongeza kuwa, "IAEA ina wakaguzi 127 nchini Iran, na waliofukuzwa walikuwa hawajaitembelea Iran kwa miaka mingi."

Kwa mujibu wa shirika la habari la IRNA, Eslami amesema kuivalia njuga kesi hiyo ya kutimuliwa wakaguzi hao wa IAEA kumetokana na hulka ya nchi hizo tatu za Ulaya ya kupenda kuingiza siasa kwenye masuala ya wakala huo; na kwamba ni sehemu ya vita vya kisaikolojia vya nchi hizo dhidi ya Iran.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI) amebainisha kuwa, nchi hizo zenye misimamo ya kiuadui dhidi ya taifa hili, zimekuwa zikisisitiza kuwa Tehran inapasa kufungamana na vipengee vya makubaliano ya JCPOA, katika hali ambayo zenyewe hazifanyi chochote, bali zimeshindwa kutekeleza ahadi ilizotoa.

 

Eslami amesisitiza kuwa, shughuli zote za nyuklia hapa nchini zinafanywa kwa kuzingatia viwango na kanuni za Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.

Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran ameeleza bayana kuwa, mafanikio ya teknolojia ya nyuklia ya Iran yanalenga kuleta amani na kutoa huduma kwa wanadamu, akisisitiza kuwa Tehran haina nia ya kuunda silaha za nyuklia.

Tags