Mkuu wa IAEA: Iran-mwanachama wa NPT, ina haki ya kurutubisha urani
-
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa IAEA
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA), amesema katika mahojiano na gazeti la Financial Times kwamba, Iran kama nchi iliyotia saini Mkataba wa Kuzuia Uenezaji wa Silaha za Nyuklia (NPT), ina haki ya kurutubisha urani.
Matamshi ya Grossi yanakuja huku mvutano ukishtadi kufuatia mashambulizi ya Israel na Marekani dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran. Kwa mujibu wa maafisa wa Iran,vituo vitatu vya nyuklia vilivyolindwa na NPT, vililengwa wakati wa mashambulizi hayo ya mwezi Juni mwaka jana.
Tehran imemkosoa Mkurugenzi Mkuu wa IAEA kwa kutolaani waziwazi mashambulizi hayo, na badala yake kushughulishwa na suala la kuendelea ukaguzi hapa nchini.
Grossi amesema wakaguzi wa IAEA wamekuwa wakisubiri kwa miezi kadhaa ili kuruhusiwa kufika katika maeneo hayo matatu muhimu ya nyuklia yaliyoshambuliwa. Viongozi wa Iran wanasisitiza kuwa, IAEA haina haki ya kutaka kukagua vituo vilivyoshambuliwa.
Maafisa wa Iran wamesema kwamba, ushirikiano wowote na shirika hilo la Umoja wa Mataifa lazima uendane na sheria iliyopasishwa na Bunge la Iran, ambayo imelipa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa mamlaka ya usimamizi wa vituo hivyo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesisitiza kwamba, Iran inaendelea kufungamana na mkataba wa NPT na kushirikiana na IAEA ndani ya mfumo wa sheria za ndani.
Kwa mujibu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran, ukaguzi umefanywa katika vituo ambavyo havikushambuliwa, na kwamba suala muhimu kwa sasa linahusu maeneo ya nyuklia ambayo yalishambuliwa kijeshi. Limesema ukaguzi wa vituo hivyo unahitaji itifaki iliyo wazi na iliyofafanuliwa.