Maambukizi ya Ebola DRC yakaribia 3,000 huku vifo vikifikia 1,269
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140140-maambukizi_ya_ebola_drc_yakaribia_3_000_huku_vifo_vikifikia_1_269
Maambukizi ya virusi vya Ebola yameongezeka kwa kasi na kufikia karibu kesi 3,000 zilizothibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku vifo vikizidi 1,260. Hali hii inajiri baada ya mamlaka za afya kuoanisha kanzidata za mikoa na zile za kitaifa, sambamba na kuripotiwa kwa makumi ya kesi mpya katika kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.
(last modified 2026-07-25T03:05:24+00:00 )
Jul 25, 2026 03:03 UTC
  • Maambukizi ya Ebola DRC yakaribia 3,000
    Maambukizi ya Ebola DRC yakaribia 3,000

Maambukizi ya virusi vya Ebola yameongezeka kwa kasi na kufikia karibu kesi 3,000 zilizothibitishwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), huku vifo vikizidi 1,260. Hali hii inajiri baada ya mamlaka za afya kuoanisha kanzidata za mikoa na zile za kitaifa, sambamba na kuripotiwa kwa makumi ya kesi mpya katika kitovu cha mlipuko wa virusi hivyo.

Taasisi ya Kitaifa ya Afya ya Jamii ilisajili kesi 2,905 zilizothibitishwa na vifo 1,269 kufikia Julai 22, ikiwa ni ongezeko kubwa kutoka kesi 2,536 na vifo 1,033 vilivyoripotiwa siku moja kabla.

Maafisa wa afya wamebainisha kuwa ongezeko hilo kubwa linaakisi zaidi ujumuishaji wa takwimu za magonjwa (epidemiology) zilizooanishwa kutoka mikoa ya Ituri na Kivu Kaskazini, na si kwamba maambukizi na vifo hivyo vyote vimetokea ndani ya saa 24.

Hata hivyo, ripoti hiyo ilirekodi kesi mpya 97 zilizothibitishwa, vifo 62 vilivyothibitishwa, na wagonjwa 13 waliopona katika kipindi cha hivi karibuni cha taarifa.

Onyo kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) ni la kutisha: Mlipuko wa sasa wa virusi vya Ebola unaoenea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo unaweza kuwa miongoni mwa milipuko mibaya zaidi kuwahi kushuhudiwa duniani.

Katika mlipuko mbaya zaidi kurekodiwa kihistoria, ugonjwa huo wa virusi unaosababisha homa ya kutokwa damu uliua zaidi ya watu 11,000 huko Afrika Magharibi kati ya mwaka 2014 na 2016. Katika mlipuko wa pili kwa ukubwa, kuanzia mwaka 2018 hadi 2020, vifo 2,287 vilirekodiwa mashariki mwa DRC.

Kwa kulinganisha, wakati wa mlipuko wa mwaka 2018 nchini DRC, ilichukua zaidi ya miezi 10 kwa idadi ya kesi kufikia 2,000. Safari hii ugonjwa huo unaenea kwa kasi kubwa sana.

Mamlaka za afya zinaonya kuwa mlipuko huu unaweza kuenea kwa upana zaidi kwa sababu eneo hilo linakabiliwa na aina adimu ya virusi vya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo haina chanjo wala matibabu yaliyoidhinishwa. Sababu ya pili ni kwamba ugonjwa huo ulikuwa ukienea kwa wiki kadhaa bila kugunduliwa rasmi kabla ya mlipuko huo kutangazwa rasmi mnamo Mei 15. Wachambuzi wananyoosha kidole kwenye udhaifu mkubwa wa mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, unaotokana na kupunguzwa kwa misaada ya afya duniani katika mwaka uliopita.