WHO: Vituo vya Ebola Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimezidiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141334-who_vituo_vya_ebola_jamhuri_ya_kidemokrasia_ya_congo_vimezidiwa
Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, vituo vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeelemewa kutokana na kuongezeka idadi ya maambukizi ya ugonjwa huuo.
(last modified 2026-09-10T02:49:04+00:00 )
Sep 10, 2026 02:47 UTC
  • WHO: Vituo vya Ebola Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimezidiwa

Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza kuwa, vituo vya Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimeelemewa kutokana na kuongezeka idadi ya maambukizi ya ugonjwa huuo.

Taarifa ya WHO imeeleza kuwa, nchi hiyo inahitaji vitanda vingine 1,600 na zaidi ya mara mbili ya idadi ya sasa ya wahudumu wa afya ili kukabiliana na mlipuko wa Ebola ulioua watu 3,226.

Kwa sasa, vituo 59 vya matibabu vina jumla ya vitanda 1,400. Shirika hilo la Afya Duniani limeeleza katika taarifa yake hiyo kwamba, vitanda vingine 1,600 vinahitajika, vikiwemo katika maeneo ya nje ya jimbo la Ituri ambako mlipuko huo ulianzia.

Idadi ya wahudumu wa afya pia inapaswa kuongezwa kutoka 4,000 hadi 9,000. Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, watu 6,686 wameambukizwa Ebola na 3,226 wamefariki dunia hadi sasa. Aidha wagonjwa wengine 819 wanatibiwa au wamewekwa katika wodi za kutengwa.

Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, Ijumaa iliyopita Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) na washirika wake walizindua mpango mpya wa sekta mbalimbali wa siku 180 unaolenga kuimarisha juhudi dhidi ya mlipuko wa sasa wa Ebola, huku mahitaji ya fedha yakikadiriwa kufikia dola bilioni 1.3 za Kimarekani.

Kwa msaada kutoka kwa Shirika la Afya Duniani (WHO), Idara ya Afya ya Afrika (Africa CDC), na washirika wengine, mpango huo unakusudiwa kuwa mwongozo wa kiutendaji wa mapambano hayo kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

Mripuko wa hivi sasa ulitangazwa mwezi Mei, na tangu wakati huo umekuwa ni janga kubwa na hatari zaidi la Ebola kuwahi kurekodiwa DRC na la pili kwa ukubwa duniani, baada ya lile janga kubwa la Ebola lililozikumba nchi za magharibi mwa Afrika katika miaka ya 2014-2016.