Kongo yaimarisha udhibiti wa serikali kwa data za uchimbaji madini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141294-kongo_yaimarisha_udhibiti_wa_serikali_kwa_data_za_uchimbaji_madini
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa inaratibu mpango wa kuimarisha udhibiti wa serikali kwa data ya kijiolojia ili kuboresha mapato ya mabilioni ya dola katika sekta ya uchimbaji madini kwa lengo la kusimamia pakubwa maendeleo ya utajiri mkubwa wa madini wa nchi hiyo.
(last modified 2026-09-08T11:04:44+00:00 )
Sep 08, 2026 11:00 UTC
  • Kongo kuimarisha udhibiti wa serikali kwa madini
    Kongo kuimarisha udhibiti wa serikali kwa madini

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imetangaza kuwa inaratibu mpango wa kuimarisha udhibiti wa serikali kwa data ya kijiolojia ili kuboresha mapato ya mabilioni ya dola katika sekta ya uchimbaji madini kwa lengo la kusimamia pakubwa maendeleo ya utajiri mkubwa wa madini wa nchi hiyo.

Chini ya mkataba wa dola milioni 180 ulioingia na kampuni ya Uhispania ya Xcalibur; Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imehamishia katika mfumo wa kidijitali rekodi za kihistoria za kijiolojia ili kuunda hifadhidata ya kitaifa ya rasilimali muhimu za madini.

Serikali ya Kongo imesema kuwa inapanga kudhibiti ufikiwaji wa data hizo kupitia mfumo wa viwango tofauti unaohusisha malipo, ikisisitiza kuwa taarifa za kijiolojia ni miundombinu muhimu ya kimkakati ya taifa.

Hatua hii inaweza kuipa Kinshasa nguvu zaidi ya majadiliano na makampuni ya uchimbaji madini, na kusaidia kuvutia uwekezaji kwa kupunguza hatari zinazohusiana na shughuli za utafutaji wa madini.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mzalishaji mkuu wa madini ya kobalti na shaba, na pia ina akiba ya lithiamu na tantalumu.

Kongo imeweka wazi sera yake hii huku ushindani kati ya Marekani na China ukiongezeka katika kupata madini muhimu.

Weledi wa mambo wanasema kuwa changamoto ya sasa kwa serikali ya Kinshasa itakuwa ni kuwa na mlingano katika kusimamia pakubwa uwazi na fursa kwa wawekezaji, huku ikihakikisha kuwa utajiri wa madini wa nchi unaleta manufaa makuu ya kiuchumi.