Algeria yakata uhusiano wake wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu
-
Algeria yakata uhusiano wake wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu
Algeria imekata uhusiano wake wa kidiplomasia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) baada ya miaka kadhaa ya kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Algeria imeishutumu Abu Dhabi kwa kuendelea kuchukua hatua ambazo inazieleza kuwa “za uchochezi au uhasama,” licha ya onyo la mara kwa mara kutoka Algiers.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria ilitangaza uamuzi huo siku ya Alhamisi, ikisema serikali ilikuwa “imetumia njia zote zilizopo” katika juhudi za kuhifadhi uhusiano wa pande mbili na nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi.
Balozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje mjini Algiers na kupewa taarifa rasmi kuhusu uamuzi huo, pamoja na kupewa muda wa saa 48 kutekeleza hatua hiyo.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria ilisema: “Kukabiliana na kuongezeka kwa hatua za uchochezi au za uhasama zinazotoka Umoja wa Falme za Kiarabu, Algeria imeonyesha uvumilivu mkubwa na hisia za juu za kuwajibika.”
Wizara hiyo imesema Algiers imekuwa ikiiwasilisha mara kwa mara wasiwasi wake kwa Imarati, na kuonya kuhusu “madhara makubwa” ambayo yanaweza kusababishwa na kile ilichokitaja kuwa “tabia ya kusikitisha na isiyo na uhalali.”
Taarifa hiyo iliongeza: “Licha ya maonyo hayo mengi, Umoja wa Falme za Kiarabu uliendelea na hatua hizo, ambazo zimefikia kiwango ambacho haziwezi tena kuchukuliwa kuwa zinakubalika au kuvumilika katika mfumo wa uhusiano kati ya mataifa mawili yenye mamlaka kamili, wala kuachwa bila majibu.”
Uhusiano kati ya nchi hizi mbili, ulianza kuyumba katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kutofautiana kuhusu masuala mbalimbali ya kikanda.
Suala kubwa lililozua mvutano kati ya nchi hizo, ni hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel. Hatua ya nchi ya Imarati ya kuiunga mkono Morocco kama mmiliki wa eneo la Sahara Magharibi ambalo pia ni jambo lingine ambalo limeharibu uhusiano wa nchi hizo mbili.