Kwa nini Ulaya imekuwa tena chombo cha mashinikizo cha Marekani?
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141356-kwa_nini_ulaya_imekuwa_tena_chombo_cha_mashinikizo_cha_marekani
Marekani na kundi la nchi tatu za Ulaya (Troika) zimeungana tena katika mkutano wa Baraza la Magavana la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika kushinikiza kupitishwa kwa azimio dhidi ya Iran na kuandaa mazingira ya kupelekwa suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
(last modified 2026-09-10T10:19:17+00:00 )
Sep 10, 2026 10:16 UTC
  • Kwa nini Ulaya imekuwa tena chombo cha mashinikizo cha Marekani?

Marekani na kundi la nchi tatu za Ulaya (Troika) zimeungana tena katika mkutano wa Baraza la Magavana la Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) katika kushinikiza kupitishwa kwa azimio dhidi ya Iran na kuandaa mazingira ya kupelekwa suala hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Hatua hii inakuja chini ya mwaka mmoja tangu utaratibu wa "kurejesha vikwazo kiotomatiki" (snapback) ulipoanzishwa, jambo linaloonyesha kuwa mashinikizo ya awali hayajatatua suala la nyuklia la Iran wala kuilazimisha Tehran kukubaliana na matakwa ya nchi za Magharibi. Sasa, badala ya kufungua njia mpya ya mazungumzo, Ulaya imerejea tena kwenye mbinu zilezile za mashinikizo, hatua ambayo inaweza kudhoofisha fursa zilizosalia za kidiplomasia kati ya Iran na Ulaya. Hata hivyo, suala la msingi si azimio lenyewe tu, bali ni msimamo wa Ulaya katika mchakato huu. Mwaka jana, kundi la 'Troika' la Ulaya, likijumuisha nchi za Uingereza, Ufaransa, na Ujerumani, lilianzisha utaratibu wa kurejesha vikwazo kiotomatiki, ili kuweka upya vikwazo vya Umoja wa Mataifa, na sasa, mataifa hayo hayo yamelipeleka tena suala la Iran mbele ya Baraza la Usalama kupitia Bodi ya Magavana. Ikiwa utaratibu huo wa "snapback" ulikusudiwa kutatua suala la nyuklia la Iran, basi kwa nini Ulaya imerudi kule kule ilikotoka? Swali hili linaonyesha kuwa sera ya mashinikizo haikufanikiwa kutatua suala hilo, na zaidi ya hayo, Iran imekataa kukubaliana na matakwa ya nchi za Magharibi.

Kwa mtazamo wa kisiasa, hatua ya hivi karibuni ya kundi la Troika pia inadhihirisha wazi utata uliopo kuhusu suala hilo. Ulaya inaelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya usimamizi wa IAEA juu ya mpango wa nyuklia wa Iran, lakini wakati huo huo inaunga mkono hatua inayoweza kufanya ushirikiano kati ya Tehran na wakala huo kuwa mgumu zaidi. Kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya vituo vya nyuklia vya Iran, uwezo wa wakaguzi wa IAEA wa kufikia maeneo yaliyoharibiwa umewekewa vizingiti, na sehemu iliyowekwa akiba ya urani iliyoratibishwa ya Iran bado haijulikani kwa wakala huo. Katika mazingira kama haya, njia ya kimantiki ya kuimarisha usimamizi ni kuweka mfumo wa kisiasa na kiusalama utakaowezesha kurejea kwa wakaguzi, badala ya kupitisha azimio jipya la kutoa mashinikizo.

Hata hivyo, Troika ya Ulaya imechagua njia tofauti kwa kuacha mazungumzo na kuamua kutoa mashinikizo zaidi na vitisho vya kupeleka suala hilo katika ngazi nyingine ya maamuzi. Matokeo ya sera ya namna hiyo yanatabirika wazi, kwa maana kuwa yanapunguza ushirikiano wa pande mbili. Mzunguko huu umejirudia kwa miaka mingi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, na kuongeza pengo kati ya Iran na Magharibi kila wakati.

Suala jingine ni kwamba Ulaya inatumia vibaya wakala wa IAEA kwa ajili ya kuendeleza malengo makubwa zaidi ya kisiasa. Kama jambo hilo lingehusu kutatuliwa masuala ya kiusalama tu, ni wazi kuwa mvutano uliopo ulipaswa kutatuliwa katika ngazi ya kiufundi kati ya Iran na wakala huo. Hata hivyo, huku Marekani na mataifa matatu ya Ulaya yakisukuma kwa wakati mmoja kupelekwa faili hilo katika Baraza la Usalama, ni dhahiri kwamba suala hilo limevuka usimamizi wa kiufundi na kuwa sehemu ya kampeni ya mashinikizo ya kisiasa dhidi ya Tehran. Hata ripoti za hivi karibuni zinaonyesha kwamba hatua yoyote inayofuata katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa itakabiliwa na kikwazo kikubwa, ikizingatiwa kwamba Russia na China zina kura ya veto. Hapa ndipo hasa udhaifu wa mkakati wa Ulaya unapoonekana wazi. Troika haiwezi kutekeleza sera ya "mashinikizo ya kiwango cha juu" bila kubeba gharama, kama Marekani inavyofanya, wala haiwezi tena kujiweka katika nafasi ya mpatanishi anayeaminika kati ya Tehran na Washington. Kwa hakika, Ulaya imekuwa chombo cha mashinikizo ya Marekani, licha ya kuwa na maslahi ya moja kwa moja ya kiusalama na kiuchumi katika kuzuia mzozo huo kuzidi kupanuka zaidi. Kadiri mvutano unavyoongezeka, ndivyo gharama kwa Ulaya inavyozidi kuwa kubwa. Sera hii haiwezi kutetewa hasa kwa kuzingatia maslahi ya Ulaya yenyewe ambapo inahitajia pakubwa kuliko upande mwingine wowote, usalama katika Asia ya Magharibi, usalama wa nishati, na kuzuia mzozo huo kupanuka. Pamoja na hayo, badala ya kusaidia kutafuta njia ya kisiasa ya kutatua mzozo uliopo, inachochea mzozo mpya juu ya msururu wa migogoro iliyopo tayari. Tabia hii bila shaka inaifanya Ulaya kuwa sehemu ya muungano unaoshinikiza Iran, badala ya kuwa mpatanishi huru asiyependelea upande wowote.

Hatimaye, hatua hii ya Troika ya Ulaya inaonyesha mapungufu na udhaifu mkubwa wa Magharibi badala ya kuonyesha nguvu yake. Ukweli ni kwamba mashinikizo yanayokaririwa huwa na matokeo mamoja tu: Kupungua zaidi kwa uaminifu wa kisiasa wa Ulaya.