US yakiri kula kipigo; Iran: Wamarekani msikubali kuwa chambo cha Israel
Afisa mmoja wa ngazi za juu wa Wizara ya Vita ya Marekani mapema leo asubuhi amekiri kwamba mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yameangamiza takriban tasisi zote za kijeshi za Marekani nchini Bahrain.
Shirika la Habari la Fars limeripoti habari hiyo na kuandika kuwa, licha ya serikali ya Marekani kuchuja mno habari za vipigo vya kijeshi inavyopata nchi hiyo kutoka kwa Iran lakini vipigo ni vikubwa kiasi kwamba leo afisa mmoja wa wizara ya vita ya Marekani (Pentagon) amelazimika kukiri uharibifu mkubwa uliosababishwa na Iran kwenye vituo vya kijeshi vya Marekani huko Bahrain.
Hung Cao, Kaimu wa Idara ya Jeshi la Wanamaji la Marekani amekiri hadharani leo Ijumaa kuwa mashambulizi ya Iran yameharibu karibu kabisa kabisa vituo vya Marekani nchini Bahrain.
Katika mahojiano na *The Epoch Times*, Cao amekiri kuwa Iran imesababisha uharibifu mkubwa kwa vituo vya kijeshi vya Marekani nchini Bahrain, ikiwa ni pamoja na miundombinu muhimu ya kupeleka na kuimarisha vikosi vya wanamaji vya Marekani.
Amesema, uharibifu uliopatikana katika makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani (US Fifth Fleet) nchini Bahrain umepunguza kwa kiasi kikubwa uwezo wa meli za Marekani kuingia bandarini.
Afisa huyo mkuu wa Pentagon amekiri pia kwamba kutokana na uharibifu huo mkubwa uliosababishwa na mashambulizi ya kulipiza kisiasi ya Iran, wafanyakazi wa meli kubwa ya kubeba ndege ya kivita *USS Abraham Lincoln* kwa hakika hawakuweza kutia nanga huko Bahrain.
Cao ameongeza kuwa Jeshi la Wanamaji la Marekani kwa sasa linatathmini iwapo litarejea na kutumia tena vituo hivyo vya kijeshi katika eneo la Asia Magharibi mara tu mzozo na Iran utakapomalizika au litaondoka kabisa kabisa.
Katika kujibu kukiri huko kwa afisa wa ngazi za juu wa wizara ya vita ya Marekani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema, "Wananchi wa Marekani hawapaswi kugeuzwa chambo cha kulipa gharama za vita vya Israel."
Shirika la Habari la Mehr limemnukuu Sayyid Abbas Araghchi akiandika hayo kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: "Tunathamini uwazi wa Hung Cao, Kaimu wa Idara ya Jeshi la Wanamaji la Marekani na tunasema, maneno yake ni sahihi kabisa; vikosi vyetu imara kwa hakika "vimesawazisha na ardhi makao makuu ya Kikosi cha Tano cha Wanamaji cha Marekani nchini Bahrain" sawa kabisa na vilivyofanya kwa vituo vingine vya kijeshi vya Marekani vinavyosaidia jinai za Washingto dhidi ya Iran. Kwa kweli, wananchi wa Marekani hawapaswi kuwa chambo cha kulipa gharama za vita vya Israel.