Iran iko tayari kuanzisha awamu mpya ya vita na kutumia mikakati mipya
-
Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia
Msemaji wa jeshi la Iran jana Alhamisi alitahadharisha kuwa Tehran itatumia mikakati na mbinu mpya ili kuifanya Marekani ishindwe kuendeleza vita iwapo mashambulio ya nchi hiyo dhidi ya miundombinu ya kusini mwa Iran yataendelea.
Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia, Msemaji wa Jeshi la Iran amesema: "Kufuatia ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano uliofanywa na Marekani sasa tunashuhudia awamu mpya ya vita." Amesema, operesheni za kulipiza kisasi za jeshi la Iran zitaendelea iwapo mashambulizi ya Marekani dhidi ya miundombinu na maeneo ya pwani ya Iran yataendelea.
"Wamarekani wanapasa kujua kuwa mchakato huu hauwezi kuendelea hivi kwa muda mrefu. Iwapo watasisitiza kuendeleza vitendo vyao vya uhasama dhidi ya maeneo ya kusini mwa nchi yetu, bila shaka tutachukua hatua mpya," ameeleza Akraminia Msemaji wa Jeshi la Iran.
Amesema "mikakati mipya imepangwa na kuandaliwa na bila shaka tutaingia uwanjani kwa namna mpya ili kumzuia adui kuendeleza vita."
Brigedia Jenerali Mohammad Akraminia ameongeza kusema "Jeshi limetumia kipindi cha kusitisha mapigano kuimarisha utayarifu wake wa kivita. Cha muhimu ni morali ya juu, hamasa na azma ya Jeshi la Anga kukabiliana na uchokozi wa adui. Kwa bahati nzuri, leo tuko katika hali bora zaidi kuliko hapo awali."