Iran yaapa kulipiza kisasi iwapo Marekani itashambulia miundombinu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140112-iran_yaapa_kulipiza_kisasi_iwapo_marekani_itashambulia_miundombinu
Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi, ameweka bayana msimamo thabiti wa Iran kwamba shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya Iran litajibiwa kwa hatua stahiki na za maamuzi dhidi ya wachokozi na wale wote wanaowasaidia.
(last modified 2026-07-23T11:52:49+00:00 )
Jul 23, 2026 11:51 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi
    Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sayyid Abbas Araghchi, ameweka bayana msimamo thabiti wa Iran kwamba shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya Iran litajibiwa kwa hatua stahiki na za maamuzi dhidi ya wachokozi na wale wote wanaowasaidia.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema: “Mafundisho yetu ya ulinzi ni dhahiri: jicho kwa jicho. Uchokozi wowote dhidi ya Iran, ikiwemo miundombinu yetu, utalazimisha jibu kali na la haraka.”

Ameongeza kwa kusisitiza: “Wale wanaochangia uchokozi huo, bila kujali aina ya usaidizi wanaotoa, watachukuliwa pia kama lengo halali la kijeshi.”

Kauli hizo kali zimekuja kufuatia vitisho vilivyotolewa na Rais wa Marekani, Donald Trump, kwamba majeshi ya Marekani yangelenga madaraja au mitambo ya umeme ya Iran ikiwa ni jibu kwa juhudi za Jamhuri ya Kiislamu za kuzuia usafirishaji haramu wa meli kupitia njia ya maji ya kimataifa.

Tamko la Waziri wa Mambo ya Nje linaendana na msimamo uliotolewa awali na kamandi kuu ya Majeshi Iran pamoja na Jeshi la Anga la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) kujibu vitisho hivyo vya uhasama.

Kamandi Kuu ya Majeshi ya Iran inayojulikana kama Khatam al-Anbiya nayo pia imetoa taarifa na kuapa kuzuia kabisa usafirishaji wa mafuta duniani kupitia Lango Bahari la Hormuz iwapo Marekani itatekeleza vitisho vyake.

Naye Kamanda wa Jeshi la Anga la IRGC, Brigedia Jenerali Seyyed Majid Mousavi, pia ameonya kuwa shambulio lolote la Marekani dhidi ya madaraja au mitambo ya umeme ya Iran litajibiwa na hatua za papo hapo za kulipiza kisasi.

Katika ujumbe wake kwenye X, amesisitiza: “Iwapo madaraja na mitambo yetu ya umeme itashambuliwa, basi giza totoro kwa washirika na wenyeji wa wauaji wa watoto ni jambo lisiloepukika.”