Mkuu wa Idara ya Mahakama: Iran Haina Uadui na nchi jirani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140144-mkuu_wa_idara_ya_mahakama_iran_haina_uadui_na_nchi_jirani
Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Gholam-Hossein Mohseni Eje’i, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina uadui wowote dhidi ya nchi jirani, akibainisha kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi hulenga vituo vilivyotumika kutekeleza mashambulizi ya Marekani katika eneo hili.
(last modified 2026-07-25T03:11:43+00:00 )
Jul 25, 2026 03:08 UTC
  • Mohseni Eje’i (kulia) na Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al- Zaidi
    Mohseni Eje’i (kulia) na Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al- Zaidi

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Gholam-Hossein Mohseni Eje’i, amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina uadui wowote dhidi ya nchi jirani, akibainisha kuwa mashambulizi ya kulipiza kisasi hulenga vituo vilivyotumika kutekeleza mashambulizi ya Marekani katika eneo hili.

Mohseni Eje’i katika mkutano wake na Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al-Zaidi, aliyeko ziarani mjini Tehran siku ya Ijumaa amesema: “Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haina uhasama wala uadui dhidi ya majirani zake, bali inawatazama kama marafiki. Siku zote tumekuwa tukiwasaidia majirani zetu, na tutaendelea kuwasaidia katika nyakati za dhiki na matatizo."

Akieleza kuwa Marekani imetumia kambi zake za kijeshi katika baadhi ya nchi jirani za Iran kama vituo vya kutekeleza mashambulizi yake na jinai zake za kivita dhidi ya taifa la Iran, Eje’i amesema: “Kwa hivyo, ni jambo la kawaida kabisa kwetu kulenga chimbuko la uchokozi wa Marekani.”

Ametoa wito kwa Waislamu na wapenda uhuru duniani kote kushirikiana ili kukabiliana na wavamizi na watawala vamizi, ili kuleta amani na utulivu katika eneo hili na kwingineko.

Akiashiria uadui wa miongo mingi wa Marekani dhidi ya Iran na sera zake za uhasama kupitia propaganda, vita vya kisaikolojia, ugaidi wa kiuchumi, pamoja na njama za kiusalama na kijeshi, amesema:

“Katika mwaka mmoja na nusu uliopita, uhasama na uchokozi wa Marekani dhidi ya taifa la Iran umefikia kilele chake. Hata hivyo, taifa la Iran na mfumo wake wa Kiislamu vimesimama imara kwa uwezo wao wote na kwa ustahamilivu mkubwa mbele ya wavamizi hawa waovu, wasaliti na wauaji wa watoto.”

Amesisitiza kuwa Iran katu haitasalimu mbele ya mvamizi kwa hali yoyote ile.

Kwingineko katika matamshi yake, mkuu huyo wa Idara ya Mahakama amepongeza ushiriki mkubwa wa wananchi wa Iraq katika hafla ya mazishi ya Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei.

Akiangazia mafungamano imara kati ya Iran na Iraq, amesisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa ushirikiano wa pande mbili, hususan ushirikiano wa kimahakama.