Mufti wa Oman: Umma wa Kiislamu umekumbwa na fitina kubwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141410-mufti_wa_oman_umma_wa_kiislamu_umekumbwa_na_fitina_kubwa
Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed Al-Khalili, amekosoa misimamo ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu kuhusu Ansarullah ya Yemen, akieleza kuwa, hali imekuwa ya hatari kutokana na kuzuka tena mapigano nchini humo.
(last modified 2026-09-13T07:21:30+00:00 )
Sep 13, 2026 07:20 UTC
  • Mufti wa Oman: Umma wa Kiislamu umekumbwa na fitina kubwa

Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed Al-Khalili, amekosoa misimamo ya baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu kuhusu Ansarullah ya Yemen, akieleza kuwa, hali imekuwa ya hatari kutokana na kuzuka tena mapigano nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Mehr likinukuu CNN Arabic, Sheikh Al-Khalili amesema kuwa kuzuka tena vita nchini Yemen, sambamba na migogoro inayoendelea Palestina, Iran na Lebanon, ni miongoni mwa mitihani na masaibu mapya yanayoikabili Umma wa Kiislamu.

Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa kijamii wa X, amesema: “Umma wa Kiislamu siku hizi umekumbwa na fitina kubwa. Mbali na masaibu na mitihani tunayokabiliana nayo Palestina, Lebanon na Iran, sasa nchini Yemen ndugu wamegeukiana na kuuana. Laiti ningejua ni kwa nini hekima ya Yemen imeshindwa kuzuia umwagaji damu na kuleta umoja!”

Ameeleza matumaini yake kwamba wananchi wa Yemen watarudi katika busara na uamuzi wa hekima, watarekebisha uhusiano wao na kujenga Yemen yenye umoja na mshikamano. Pia ametoa wito kwa watu wenye nia mbaya au wale wanaochochea mgawanyiko kwa sababu ya ujinga na uzembe, wasiwagawanye Wayemeni wala kupandikiza chuki na uadui miongoni mwao.

Mufti huyo wa Oman amesema kwamba, kama anavyosikitishwa na hali ya ndugu zao nchini Yemen, vivyo hivyo amesikitishwa na kauli za baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu. Amesema baadhi ya wanazuoni hao wamezungumza dhidi ya kundi ambalo, tangu kuanzishwa kwake, limekuwa likisimama kwa nguvu na azma dhidi ya utawala wa Kizayuni, na limejitolea kwa mali na maisha katika juhudi za kuikomboa misikiti na maeneo matakatifu ya Kiislamu pamoja na kuwaunga mkono wananchi wa Palestina wanaodhulumiwa.

Mufti Ahmed Al-Khalili amesema, haikupaswa kutolewa kauli za aina hiyo, akisisitiza kwamba katika kipindi hiki nyeti, Umma wa Kiislamu haupaswi kupuuza mapambano dhidi ya uvamizi huu hatari na badala yake kujishughulisha na masuala ya pembeni.

Kwa hiyo, amewataka wanazuoni wakuu wa Kiislamu katika kipindi hiki wasijishughulishe na jambo lolote zaidi ya suala lao la msingi, yaani ukombozi wa maeneo matakatifu ya Kiislamu yaliyonyakuliwa, na kutumia hekima yao ya muda mrefu kutafuta suluhisho la tatizo hilo kabla halijapanuka na kuwa gumu zaidi kulitatua.

Amehitimisha kwa kusema kwamba, hali imefikia kiwango kikubwa cha hatari, kiasi kwamba hata mtu mwenye subira hawezi kufanya lolote zaidi ya kuhuzunika sana.