Ulimwengu wa Spoti, Dec 15
Hujambo mpenzi mskilizaji na karibu tuangazie baadhi ya matukio makubwa yaliyojiri viwanjani ndani ya siku saba zilizopita kote duniani.
Iran yang'ara katika mashindano ya AYPG Dubai
Iran imeibuka mshindi wa pili katika Michezo ya Vijana Walemavu wa Asia (AYPG) ya 2025 huko Dubai, katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Kikosi cha Iran chenye wanamichezo 194 kilikusanya jumla ya medali 262, zikiwemo dhahabu 76, fedha 96, na shaba 88, katika mashindano hayo yaliyofanyika kuanzia Desemba 10 hadi 13. Waogeleaji wa Iran walishinda medali 104, huku wanariadha wakichota medali 82 katika vitengo mbalimbali.
Mashindano hayo yaliwaleta pamoja wanariadha na wanamichezo wapatao 1,500 kutoka mashirikisho 35 ya kitaifa kote Asia. Uzbekistan iliongoza jedwali la medali kwa medali 153, zikiwemo medali 99 za dhahabu za kuvutia. Japan ilimaliza ya tatu kwa jumla ya medali 77, zikiwemo dhahabu 40, fedha 25, na shaba 12. Iran ilikuwa imeongoza orodha ya medali katika toleo lililopita mwaka wa 2021 Bahrain, ikishinda medali 122, zikiwemo dhahabu 44.
Timu ya mpira wa wachezaji wenye matatizo ya kuona ya wasichana ya Iran iliibuka kidedea kwenye mashindano hayo ya Vijana wa Asia baada ya kuigaragaza Thailand katika mechi ya fainali na kushinda medali ya dhahabu. Iran, ambayo ilishinda medali ya fedha katika duru iliyopita ya mashindano hayo, iliicharaza Thailand mabao 6-2 katika ngoma ya fainali ya goalball kwa wanawake iliyopigwa Jumamosi. Kocha mkuu wa timu hiyo ya vijana ya Iran, Mojgan Karbi, ametangaza kuitunuku medali hiyo ya dhahabu kwa mashahidi wa vita vya siku 12 vya kutwishwa via Israel dhidi ya Iran Juni mwaka huu. Karbi alisema, "Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano ya wanawake, tulifanikiwa kupata ubingwa huu. Katika matoleo yaliyopita, tulimaliza kama washindi wa pili au katika nafasi ya tatu, lakini katika toleo hili, kupitia juhudi na mshikamano wetu, tulikuwa mabingwa. Tunalikabidhi taji hili kwa mashahidi wa vita vya siku 12 vilivyotwishwa nchi yetu." Timu ya wanaume ya goalball ya Iran kwa upande wao ilikubali medali ya shaba baada ya kuishinda Thailand mabao 15-7 siku ya Jumamosi katika mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu. Wakati huo huo, timu ya taekwondo ya walemavu ya Iran imeibuka kidedea baada ya kushinda medali tisa za kupendekeza katika mashindano hayo ya AYPG, zikiwemo nne za dhahabu, tatu za fedha, na mbili za shaba. Hali kadhalika, timu ya tenisi ya mezani ya wanaume ya Iran ilitwaa ubingwa katika mashindano hayo ya kibara siku ya Jumamosi. Arsham Ramezani na Ali Rasti waliibuka washindi dhidi ya Huang Ren Ting na Su Jin Sian kutoka China Taipei kwa kuwalaza alama 3-2 (10-12, 12-14, 12-10, 11-7, 12-10) katika fainali ya kategoria ya wachezaji wawili kila upande, kwa vijana wenye chini ya miaka 23.
Kabla ya hapo, Wairani Abolfazl Khosravi na Mohammad Parsa Sohrabi walishinda medali mbili zaidi za dhahabu katika Michezo ya Vijana wa Asia ya Dubai 2025. Khosravi alishinda medali ya dhahabu katika mchezo wa kurusha kirungu (club throw) kwa upande wa wanaume, safu za F31, F32, F51 kwa kurusha umbali wa mita 23.9. Naye Sohrabi alishinda medali ya dhahabu katika urushaji kisahani (discus) kategoria za F42, F43, F44, F45, F46, F47, F61, F62, F63, F64 kwa kurusha umbali wa mita 38.99.
Voliboli ya Wanafunzi; Iran bingwa
Timu ya voliboli ya vijana wa kiume ya Iran imeibuka bingwa baada ya kuichakaza China Taipei seti 3-1 (15-25, 25-18, 25-22, 25-17) katika fainali ya Mashindano ya Dunia ya Voliboli ya Shule ya ISF kwa vijana wenye chini ya miaka 15 ya 2025 siku ya Ijumaa. Iran ilikuwa imewashinda Nigeria, China, Saudi Arabia, China na India wakiwa njiani kuelekea mechi ya fainali. Timu ya mabanati ya Iran ilimaliza katika nafasi ya sita katika mashindano hayo.
Mashindano ya Voliboli ya Shule ya Dunia ya ISF U15 2025 yalifunguliwa rasmi mnamo Desemba 5 katika Gymnasium ya Shangluo, China na kuzileta pamoja timu 30 kutoka kwa wajumbe 17 kwa siku nane za mashindano ya kimataifa ya michezo ya shule na ubadilishanaji wa kitamaduni. Mashindano ya Voliboli ya Shule ya Dunia ya ISF yaliyofanyika kwa mara ya kwanza mwaka wa 1972, ni michuano ya voliboli ya shule ya kiwango cha juu zaidi duniani kote.
Dondoo za Hapa na Pale
Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amempongeza Soraya Aghaei kwa kuteuliwa kuwa mwanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), baada ya Jamhuri ya Kiislamu kukosa fursa kama hiyo kwa takriban miaka 21.
Sambamba na mnasaba wa kuadhimisha mazazi ya Bibi Fatimatu Zahra SA, na Siku ya Kitaifa ya Mama hapa nchini, Rais Pezeshkian, katika ujumbe kwenye akaunti yake ya X, alimpongeza Aghaei kwa kuipaisha Iran katika jukwaa hilo la kimataifa la michezo.
Kwengineko, Kocha Mkuu wa timu ya taifa ya Algeria, Madjid Bougherra, ametangaza rasmi kuachana na kikosi hicho siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya kikanda ya AFCON, kufuatia kuondolewa kwa kikosi chake kwenye michuano ya Kombe la Waarabu la FIFA. Bougherra, ambaye mkataba wake ulikuwa ufike tamati mwezi Desemba mwaka huu (2025), amesema kuwa safari yake na timu ya taifa ya Algeria imefikia mwisho. Akizungumza baada ya matokeo hayo, kocha huyo alibainisha kuwa ametoa mchango wake wote kwa timu na sasa ni wakati wa uongozi mpya kuendeleza jukumu hilo. Kocha huyo ataendelea kukumbukwa kwa mafanikio makubwa aliyoyapata akiwa na Algeria, hususan kuiongoza timu hiyo kutwaa ubingwa wa FIFA Arab Cup mwaka 2021, mafanikio yaliyomweka katika historia ya soka la taifa hilo. Uamuzi wa Bougherra unakuja wakati nyeti kwa Algeria, ikijiandaa kushiriki AFCON, huku mashabiki na wadau wa soka wakisubiri kwa hamu kujua ni nani atakayechukua nafasi yake kuiongoza timu hiyo katika mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika.
Wakati huo huo, Kocha Mkuu wa Timu ya Taifa ya Ivory Coast, Emerse Faé, ametangaza rasmi orodha ya wachezaji 25 watakaoiwakilisha nchi yao katika kipute cha AFCON 2025 huko Morocco. Tangazo hilo hata hivyo limekuwa pigo kwa mashabiki wengi waliokuwa na matumaini ya kumwona kiungo wa Yanga SC, Pacôme Zouzoua, akipata nafasi katika kikosi hicho. Taarifa rasmi zimebaini kwamba, Zouzoua hatawezi kujiunga na timu hiyo, licha ya kiwango chake bora katika Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kwengineko, wafanyakazi wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke walishiriki mbio za TIA Marathon 2025 zilizofanyika Jumamosi ya Desemba 13, katika Chuo cha Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Dar es Salaam zikiwa na lengo la kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum pamoja na kupambana na magonjwa yasiyo ya kuambukiza. Katika mbio hizo kulikuwa na mbio za kilomita 5, 10 na 21, huku TANESCO Mkoa wa Temeke wakishiriki mbio za kilomita 5, 10 kwa lengo la kutoa mchango wa kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum, wakiwemo akina mama wanaojifungua wakiwa wanaendelea na masomo chuoni. Mbio za TIA Marathoni 2025 zilibeba kaulimbiu ya “Kimbia, Hamasisha, Saidia.”
Mbali na hayo, baada ya matokeo ya karibuni kwenye soka la Ulaya, shirika la Opta lilitoa utabiri wake wa hivi punde, likisisitiza kuwa Arsenal ipo katika nafasi kubwa zaidi ya kushinda taji lao la kwanza la Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya msimu huu. Gunners wamepewa nafasi kushinda taji hilo kwa ubashiri wa 23.31%, huku Bayern Munich wakiwa wa pili kwa nafasi ya 19.01%. Wabavaria walirudi kutoka kwa kushindwa kwao na Arsenal na kuishinda Sporting Lisbon nyumbani. Arsenal iliendeleza mwanzo wao mzuri wa Ligi ya Mabingwa msimu huu, ikiishinda Club Brugge 3-0 na timu ya pili Jumatano usiku. Noni Madueke alifunga mabao mawili, la kwanza likiwa la kupiga kelele, na kuisaidia Gunners kupata ushindi rahisi nchini Ubelgiji.

Aidha Arsenal wameendelea kutuama kileleni mwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupata ushindi wa magoli 2–1 dhidi ya Wolves walioko mkiani ugani Emirates, ingawaje haikuwa lelemama. Namna Guners walivyopata ushindi huo wa wikendi, imeacha maswali mengi kuliko majibu kuhusu uwezo wao wa kutwaa ubingwa msimu huu. Kile kilichotarajiwa kuwa mchezo laini wa nyumbani, kiligeuka kuwa mechi ya taharuki na roho juu, kuashiria kuwa kuna mapungufu yanayohitaji kufanyiwa kazi. Ushindi huo umefikisha Arsenal pointi 36 na kudumisha pengo lao kileleni, lakini kuhitaji mabao mawili ya kujifunga kutoka kwa Wolves ili kuwafunga timu ambayo haijashinda mipepetano 16 mfululizo si ishara ya wazi ya mabingwa watarajiwa.
Nchini Uhispania, kiwango duni cha Real Madrid chini ya Xabi Alonso kiliendelea huku Manchester City wakitoka nyuma na kuwashinda huko Bernabeu. Rodrygo aliwaongoza katika dakika ya 28, lakini Nico O'Reilly alisawazisha muda mfupi baadaye, baada ya Thibaut Courtois kufanya kazi ya kuokoa mpira. Erling Haaland alifunga kupitia mkwaju wa penalti baada ya kuangushwa na Antonio Rudiger. Tukiwa bado Uhispania, mabingwa watetezi Paris Saint-Germain walilazimishwa sare tasa na Athletic Bilbao, huku Barcelona ikiifunga Eintracht Frankfurt mabao 2-1, yaliyotiwa kimyani kimuujiza na Jules Kounde. Arne Slot alipata muda wa kupumzika baada ya kupanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Inter Milan kutokana na penalti ya dakika za mwisho kutoka kwa Dominik Szoboszlai. Mkufunzi wa Barca, Hans Flick anasema cha mno ni kwamba wameondoka na alama 3, ingawaje anakiri mchezo ulikuwa mgumu. Kwa mujibu wa bishara za Opta, PSG wako katika nafasi ya tatu ya kutwaa ubingwa, huku uwezekano wao wa kushinda ukiwa wa asilimia 13.53 huku Manchester City wakiwa na nafasi ya asilimia 10.27. Kompyuta hiyo kubwa pia imetabiri timu zitakazofuzu kwa Raundi ya 16 kiotomatiki. Arsenal na Bayern Munich tayari zimefuzu, na inatabiriwa wataungana na Manchester City, PSG, Real Madrid, Liverpool, Atletico Madrid na Atalanta. Atalanta iliishinda Chelsea 2-1 mjini Bergamo na kupanda hadi nafasi ya tano kwenye jedwali zikiwa zimesalia michezo miwili. Arsenal yaunga mkono kushinda Ligi Kuu. Katika Ligi Kuu ya Uingereza, Opta pia inabashiri Arsenal kushinda kwa mara ya kwanza tangu 2004 licha ya kupoteza dhidi ya Aston Villa.
Salman kununu Barcelona kwa mabilioni ya euro?
Na tunatamatisha kwa tetesi hii kwamba, Mrithi wa Ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman anaripotiwa kuwa tayari kutoa euro bilioni 10 kuinunua klabu ya soka ya Uhispania ya Barcelona. Mwandishi wa habari wa tovuti ya El Chiringuito, Francois Gallardo amesema hayo kwenye ukurasa wake rasmi wa mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, wanachama wa klabu hiyo wanaoshiriki katika uchaguzi wa rais wa klabu hiyo wanaweza ama kukubali au kuzuia mauzo hayo.
Habari hii imesambaa kwa kasi kama moto wa kichaka kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye vyombo vya habari duniani. Hapo awali, Joan Laporta alitangaza kwamba hana azma ya kugombea tena urais wa klabu hiyo mashuhuri ya soka duniani. Muhula wake wa sasa unamalizika mwaka wa 2027.
……………….TAMATI……………