Iran yaonya: Hatutaanzisha vita, lakini tutajibu vikali uvamizi wowote
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136844-iran_yaonya_hatutaanzisha_vita_lakini_tutajibu_vikali_uvamizi_wowote
Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitaanzisha vita, lakini itatoa jibu zito kwa kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya nchi hii.
(last modified 2026-02-20T09:48:55+00:00 )
Feb 20, 2026 09:48 UTC
  • Iran yaonya: Hatutaanzisha vita, lakini tutajibu vikali uvamizi wowote

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amesisitiza kwamba, Jamhuri ya Kiislamu haitaanzisha vita, lakini itatoa jibu zito kwa kitendo chochote cha uchokozi dhidi ya nchi hii.

Amir Saeid Iravani amesema hayo katika barua aliyoitumwa jana Alkhamisi kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais wa Baraza la Usalama la umoja huo, siku moja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kutishia kwamba Washington inaweza kuhitaji kutumia Kisiwa cha Diego Garcia cha Bahari ya Hindi, ambacho kina kambi ya pamoja ya kijeshi ya Uingereza na Marekani, kuishambulia Iran.

Ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakariri kusema na kutilia msisitizo kwamba, haitafuti mvutano wala vita, na wala haitaanzisha vita vyovyote. "Hata hivyo, ikiwa itashambuliwa kijeshi, Iran itajibu kwa nguvu na kwa mlingano sawa, katika kutekeleza haki yake ya asili ya kujihami chini ya Kifungu cha 51 cha Hati ya Umoja wa Mataifa," amesisitiza Iravani.

Kadhalika mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa, ikiwa kutatokea uvamizi wowote wa kijeshi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu, kambi zote za kijeshi, vifaa, silaha, na milki za "jeshi vamizii" zitakuwa "shabaha halali" katika operesheni za kulipiza kisasi za Iran.

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameonya kuwa, Marekani, itawajibika na kubeba dhima kwa matokeo yoyote "yasiyotabirika na yasiyoweza kudhibitiwa ya uchokozi wowote dhidi ya Iran."

Aidha amelaani vitisho vya Trump vya kutumia nguvu za kijeshi dhidi ya Iran, na kuvitaja kama ukiukaji mkubwa wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa; akisisitiza kuwa, uchokozi wowote dhidi ya Iran utalitumbukiza eneo lote la Asia Magharibi katika mzunguko mpya wa mgogoro na ukosefu wa utulivu.