Mamia ya watu wanaandamana Afrika Kusini kupinga chuki dhidi ya wageni
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i140538-mamia_ya_watu_wanaandamana_afrika_kusini_kupinga_chuki_dhidi_ya_wageni
Mamia ya watu wameandmana katika miji mbalimbali nchini Afrika Kusini wakitaka kukomeshwa ghasia dhidi ya wahamiaji, ambazo zimewalazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia nchi hiyo.
(last modified 2026-08-09T11:09:01+00:00 )
Aug 09, 2026 11:04 UTC
  • Mamia wameandamana Afrika Kusini kupinga chuki dhidi ya wahamiaji.
    Mamia wameandamana Afrika Kusini kupinga chuki dhidi ya wahamiaji.

Mamia ya watu wameandmana katika miji mbalimbali nchini Afrika Kusini wakitaka kukomeshwa ghasia dhidi ya wahamiaji, ambazo zimewalazimisha makumi ya maelfu ya watu kukimbia nchi hiyo.

"Inatosha sasa; hatuwezi kukaa kimya na kutazama huku wenzetu wakishambuliwa na biashara zao zikiporwa. Hali hii lazima ikome," alisikika akisema Phakamile Johnny alipozungumza na shirika la habari la Anadolu.

Naye Thuli Nkadimeng, mwanaharakati wa masuala ya wahamiaji amesema akiwa katika maandamano ya mshikamano huko Johannesburg kwamba wanataka wale wote wanaochochea vurugu na vitisho dhidi ya raia wa kigeni wawajibishwe.

Walioandaa maandamano hayo pia wameitaka serikali ya Afrika Kusini iache kuwafukuza na kuwarejeshwa makwao wahamiaji.

Mashirika ya kiraia zaidi ya 60 yanayowakilisha jamii mbalimbali kote Afrika Kusini na barani Afrika yameshiriki kwenye maandamano yaliyofanyika Johannesburg, Pretoria, Cape Town na Durban kwa shabaha ya kudai haki na kukomesha vitendo vya chuki dhidi ya wageni.

Makundi ya wananchi wa Afrika Kusini yanaojichukulia sheria mikononi tangu mwezi Aprili mwaka huu yamekuwa yakiandamana kupinga wahamiaji nchini humo yakitaka kuwa wahajiri wasio na vibali halali vya makazi waondoke nchini humo.

Wamekuwa wakipita nyumba kwa nyumba wakiwataka wahamiaji kutoka nchi za Afrika na Asia kuwaonyesha pasipoti na nyaraka zao za utambulisho, hatua ambayo serikali ya Afrika Kusini imeilaani vikali.

Wakimbizi na wahamiaji nchini Afrika Kusini wanasema kuwa kila siku hukumbana na matukio ya unyanyasaji, vitisho, uporaji na kufungwa biashara zao.