Tabia za Marekani Kudumisha Mvutano katika uhusiano wake na Iran
Mwenendo wa Rais Donald Trump wa Marekani kuhusiana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran unachochea kuendelea kwa mvutano na uhasama katika uhusiano wa Washington na Tehran.
Ingawa hivi karibuni Trump alitangaza mipango ya kutekeleza shambulio kubwa na kali dhidi ya miundombinu ya Iran, amedai tena kuwa aliahirisha shambulio hilo kutokana na ombi la baadhi ya nchi za eneo na kwa kuzingatia utayari wa Iran wa kufanya mazungumzo.
Mbali na Iran kukanusha madai ya Trump kwamba ilikuwa imeomba kufanya mazungumzo, nchi za eneo, ikiwemo Saudi Arabia, zimetoa wito wa kufanyika mazungumzo na Iran na kusisitiza kuepukwa mashambulizi dhidi ya miundombinu. Bila kujali iwapo shambulio jipya la ukubwa uliotajwa na Trump litatokea, au kama mazungumzo mapya yatafanyika, ushahidi unaonyesha kuwa mwenendo wa Marekani unachochea hali ya mgogoro unaoendelea katika uhusiano wake na Iran.
Hadi sasa, Marekani haijafikia malengo yake ya kimkakati kuhusu Iran kupitia hatua za kijeshi, na kwa sasa inafuatilia malengo mahususi matatu kuhusiana na nchi hii. Lengo kuu la Marekani ni kutaka kuitwisha Iran matakwa yake ya kisiasa. Marekani haijashindwa tu kufikia malengo yake ya kijeshi, bali sasa inakabiliwa na msimamo thabiti wa Iran wa kutaka kuwepo kwa mipango mipya ya kiusalama ya kusimamia Lango-Bahari la Hormuz. Hali hii ni mbaya zaidi kwa Marekani hata kuliko kushindwa kijeshi, ikizingatiwa kuwa lango hilo lilikuwa wazi kabla ya kuanza vita, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwahi kuzungumzia mipango mipya ya kiusalama kuhusiana na lango hilo. Katika muktadha huu, Trump anakabiliwa na ukosoaji mkubwa ndani na nje ya Marekani. Ingawa Trump anadai kupata ushindi dhidi ya Iran, akijibu hoja za wakosoaji wanaomwona kama aliyeshindwa katika vita hivi, anahitaji kulazimisha matakwa yake ya kisiasa dhidi ya Iran ili kuwanyamazisha wakosoaji hao kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani. Lengo jingine muhimu linahusiana na mtazamo wa pamoja wa Marekani na utawala wa Kizayuni kuhusu udharura wa Israel kudumisha ubora wa kijeshi katika eneo. Utawala wa Kizayuni unalenga waziwazi kuwa nguvu kuu ya kijeshi katika Asia Magharibi, na ubabe wa Israel katika eneo pia unaendana na maslahi ya Marekani. Wataalamu wanaamini kuwa mkakati wa Trump unalenga kudhoofisha nguvu na uwezo wa Iran wa kuzuia mashambulizi (deterrence) ili kulinda nafasi ya Israel kama nguvu kuu ya kijeshi katika eneo. Mzozo wa Marekani na Iran hauhusiani tu na mpango wa nyuklia wa Iran bali lengo kuu ni kuhakikisha kuwa Israel inashikilia nafasi ya juu katika eneo na kwamba hakuna taifa jingine litakalokuwa na uwezo wa kuipinga. Katika muktadha wa nadharia ya uhalisia wa mashambulizi (offensive realism), mwenendo wa sasa wa Israel unaweza kufafanuliwa kama wa nguvu ya kikanda inayotaka kubadili hali iliyopo (revisionist power), nguvu inayofuatilia usalama si kwa kukubali uwiano wa nguvu, bali kwa kuvuruga mara kwa mara uwiano huo ili kujinufaisha yenyewe. Lengo la tatu la Marekani ni kudhoofisha uwezo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuigeuza kuwa taifa dhaifu. Kwa hakika, suala linaloinyima usingizi Marekani si "Iran yenye silaha za nyuklia," bali ni "Iran yenye nguvu na uwezo mkubwa." Marekani inaiona Iran kama nchi pekee katika eneo la Asia Magharibi inayosisitiza udharura wa kujitawala na kutegemea uwezo wake wa ndani wa kujilinda, msimamo unaoweza kuigwa na mataifa mengine ya eneo, na hivyo kuhatarisha maslahi ya Marekani katika eneo, kwa kutaka kuondoa utegemezi wao wa kiusalama kwa Washington. Mapambano makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya Marekani na Israel katika vita vya karibuni yamedhihirisha zaidi uwezo wake wa kujilinda dhidi ya hujuma ya maadui. Hivyo, Washington inaamini kuwa ni lazima iishambulie na kuiletea madhara ili kudhoofisha uwezo wake na kuizuia isiendelee kuwa taifa lenye nguvu kubwa ya kijeshi.
Hivyo, kwa kuzingatia mapambano ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya hatua za kichokozi za Marekani katika nyanja za kisiasa na kijeshi, kuendelea kwa mwenendo huu wa Washington kunaweza kuchochea kuongezeka mvutano katika uhusiano wake na Iran, pamoja na kueneza mzozo huo katika eneo zima la Asia Magharibi na hata maeneo mengine.