Ufichuzi kuhusu kisingizio bandia kilichotumiwa na Trump kuishambulia Iran
Joe Kent, afisa wa zamani katika utawala wa Trump, amekiri kuwa madai kuhusu Iran kutengeneza silaha za nyuklia ni mbinu ya kipropaganda tu iliyotumika kwa ajili ya kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya Iran.
Joe Kent, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kupambana na Ugaidi katika utawala wa Trump, ameashiria kauli ya uongo ya Trump kwamba Iran ilikuwa inakaribia kutengeneza silaha za nyuklia, na kusisitiza kuwa madai hayo hayakuwa chochote isipokuwa kisingizio cha propaganda kwa ajili ya kuanzisha shambulio la kijeshi la pamoja la Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran. Kent ambaye mwenyewe ni afisa mwandamizi wa usalama katika utawala wa Trump na mkongwe wa Kikosi Maalum cha Marekani, amejibu kupitia mtandao wa X madai ya rais wa Marekani kwamba Iran ilikuwa imesalia na muda wa "wiki mbili hadi nne" kabla ya kutengeneza silaha za nyuklia. Amesisitiza kwamba: "Iran haikuwa inatuma magaidi Marekani wala kutengeneza silaha za nyuklia. Dhana kwamba Iran ilikuwa karibu kutengeneza silaha za nyuklia ili kutushambulia ni sawa na madai ya zama za Bush kuhusu Iraq, mkakati wa propaganda tu."
Akibainisha kuwa licha ya ukweli huu wote lakini leo tunashuhudia madai hayo hayo yakitumika kuhalalisha vita vya kichokozi vya Marekani dhidi ya Iran, amesisitiza kuwa Washington ina fursa ya kujifunza kutokana na historia ya hivi karibuni, ambapo badala ya kuingiza wanajeshi wa Marekani katika hatua nyingine ya uchokozi yenye umwagaji damu na isiyo na lengo maalum, inapaswa kutumia fursa hii kujiepusha na vita vya namna hiyo.
Ufichuzi wa Joe Kent kuhusu madai yasiyo na msingi ya Trump una vipengele kadhaa. Kwanza, maudhui ya ufichuzi huu yanaendana na msimamo wa pamoja wa jamii ya intelijinsia ya Marekani. Kent amefichua kuwa kabla ya vita hivyo, jamii ya intelijinsia ya Marekani, ikiwemo CIA, ilikuwa na mtazamo wa pamoja kwamba Iran haikuwa ikitengeneza silaha za nyuklia. Amesema: "Mojawapo ya mambo ya kusikitisha kuhusu vita hivi ni kwamba, kabla ya kuanza kwake, mashirika ya kijasusi ya Marekani yalikuwa na msimamo wa pamoja kwamba Iran haikuwa ikitengeneza silaha za nyuklia." Kauli hizi zinaonyesha kuwa mfumo wa kijasusi wa Marekani haukushindwa tu kuthibitisha madai ya kuwepo tishio la karibu la nyuklia, bali ulipinga vikali madai hayo.
Sababu ya pili katika muktadha huu ni kuwepo kwa fatwa ya kidini inayopinga silaha za nyuklia. Kenneth alitaja mojawapo ya sababu zilizoandikwa na kufafanuliwa kwa uwazi mkubwa zinazoelezea upinzani wa Iran dhidi ya silaha za nyuklia na kusema: Fatwa iliyotolewa na Ayatollah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ilitangaza wazi kuwa utengenezaji na matumizi ya silaha za maangamizi ya umati ni haram, tangu mwaka 2004. Amesisitiza kuwa: "Hatukuwa na taarifa zozote za kijasusi zilizoashiria kuwa fatwa hiyo ilikuwa imevunjwa au ilikuwa karibu kufutiliwa mbali." Suala la tatu katika muktadha huu ni nafasi ya utawala wa Kizayuni katika mchakato wa kuchukuliwa maamuzi wa serikali ya Trump kuhusu shambulio dhidi ya Iran. Kent amesema waziwazi kwamba "utawala wa Kizayuni ndio uliosukuma uamuzi wa kuanzisha vita hivi" na kuwa Marekani iliingia katika mzozo huo kutokana na mashinikizo ya lobi za Kizayuni. Katika barua yake ya kujiuzulu, Keny aliandika: "Ni wazi kuwa tulianzisha vita kutokana na mashinikizo ya Israel na makundi yake ya ushawishi nchini Marekani." Kauli hizi zinafichua pande mpya za ushawishi wa kigeni katika maamuzi ya kimkakati ya Marekani.
Mambo yaliyofichuliwa na Joe Kent yana taathira kadhaa.
Kwanza, yamedhoofisha uhalali wa maelezo rasmi yanayotolewa na White House. Kauli za Kent, zikitoka kwa afisa wa ngazi ya juu zaidi kuwahi kujiuzulu kutokana na suala la vita dhidi ya Iran, zimetoa changamoto kubwa kwa maelezo rasmi ya serikali ya Trump. Amesisitiza kuwa Iran haikuwa tishio "lililokuwa karibu kutokea" kwa Marekani. Hili linakinzana na hoja ya Trump ya kuhalalisha vita hivi, kama hatua ya "kuwalinda wananchi wa Marekani dhidi ya vitisho vilivyokuwa karibu kutokea kutoka kwa utawala wa Iran."
Suala la pili ni kufanana madai yaliyotolewa kuhusiana na vita vya Iran na hali iliyojitokeza wakati wa vita vya Iraq. Kent amelinganisha waziwazi madai ya Trump na madai ya uongo ya utawala wa George W. Bush kuhusu silaha za maangamizi ya umati nchini Iraq. Ameonya kuwa Vita vya Iraq vilisababisha vifo vya takriban wanajeshi 5,000 wa Marekani, vikaacha maelfu ya wengine wakiwa vilema, na kugharimu zaidi ya dola trilioni tatu, huku akitahadharisha dhidi ya kujirudia kwa "hali hiyo hiyo yenye madhara makubwa."
Suala la tatu ni kupungua kwa imani ya umma kwa mashirika ya kijasusi ya Marekani. Kufichuliwa ukweli kwamba jamii ya intelijensia ilipinga hadharani mtazamo wa Rais, kumeathiri vibaya sana itibari na uaminifu wa taasisi za intelijensia za Marekani pamoja na mchakato wa kufanya maamuzi nchini humo. Kent amesisitiza kuwa "baadhi ya watu muhimu wanaohusika na kufanya maamuzi hawakuruhusiwa kutoa maoni yao kwa Rais" na kwamba "hakukuwa na mjadala wa kina kabla ya kufanyika mashambulizi hayo."
Sababu ya nne ni kuongezeka mvutano wa kisiasa ndani ya Marekani. Kujiuzulu kwa Kent, hatua iliyofuatiliwa sana kitaifa na kimataifa, na ufichuzi uliofuatia vilionyesha wazi migawanyiko mikubwa iliyopo miongoni mwa washirika wa Trump. Pamoja na hayo White House ilitupilia mbali madai yake kwa kuyaita "matamshi ya chuki dhidi ya Mayahudi," huku Trump akimwelezea kama mtu "asiye imara katika masuala ya usalama." Aidha, FBI ilianzisha uchunguzi dhidi ya Kent kwa tuhuma bandia za kuvujisha taarifa za siri. Ni wazi kuwa kauli za Joe Kent zinafichua pande fiche za mchakato wa maamuzi kuhusu vita vya kichokozi vya Marekani dhidi ya Iran. Kwa kuashiria makubaliano ya jamii ya intelijensia, fatwa ya kidini ya Iran na kutokuwepo kwa tishio lolote la karibu, ameonyesha kuwa suala la nyuklia lilikuwa kisingizio tu cha propaganda kilichotumiwa kwa ajili ya kuanzisha vita vya tatu vya kulazimishwa dhidi ya Iran. Ufichuzi huu haudhoofishi tu simulizi rasmi ya White House, bali pia unatahadharisha kuhusu matokeo yenye maafa yanayofanana na vita vya Iraq yanayoweza kutokea dhidi ya Marekani, jambo linaloweza kuwa na taathira kubwa hasi kwa imani ya umma kuhusu mashirika ya intelijensia ya Marekani na maamuzi ya kimkakati ya nchi hiyo katika siku zijazo.