Rais Pezeshkian: Iran haifanyi mazungumzo iwe imezungumza tu, inataka tija inayoonekana
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i136772-rais_pezeshkian_iran_haifanyi_mazungumzo_iwe_imezungumza_tu_inataka_tija_inayoonekana
Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza kwamba, mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja inayofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yako chini uangalizi kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na ametupilia mbali dhana ya kushiriki Iran katika "mazungumzo kwa ajili ya kuzungumza tu."
(last modified 2026-02-18T11:06:12+00:00 )
Feb 18, 2026 11:06 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran haifanyi mazungumzo iwe imezungumza tu, inataka tija inayoonekana

Rais Masoud Pezeshkian amesisitiza kwamba, mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja inayofanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani yako chini uangalizi kamili wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na ametupilia mbali dhana ya kushiriki Iran katika "mazungumzo kwa ajili ya kuzungumza tu."

"Mazungumzo haya yanafanywa kwa uratibu kamili na idhini kutoka kwa Kiongozi," amebainisha Rais Pezeshkian katika mkutano na viongozi kadhaa wa kidini uliofanyika hapa jijini Tehran.

"Lengo letu ni kutatua masuala kwa dhati, si kushiriki katika mazungumzo kwa ajili ya kuzungumza tu. Tunafuatilia kwa uzito kupata matokeo yanayoonekana na tunatumai mchakato huu utapelekea kupatikana matokeo halisi," amesisitiza Rais wa Iran.

Jana Jumanne, duru ya pili ya mazungumzo mapya ya nyuklia kati ya Iran na Marekani ilihitimishwa mjini Geneva, Uswisi.

Mazungumzo hayo yasiyo ya ana kwa ana yalifanyika katika ubalozi wa Oman mjini humo kwa usimamizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Albusaidi.

Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika mjini Muscat, Oman mapema mwezi huu.

Imeelezwa kwamba, mazungumzo ya jana yalishirikisha pia wataalamu wa masuala ya nyuklia, sheria, na uchumi. 

Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje Sayyid Abbas Araghchi wa Iran umesema "hatua nzuri zimepigwa," huku ukisisitizia haja ya mchakato huo kupelekea kuondolewa vikwazo haramu na vya upande mmoja ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu na Marekani.../