Kwa kuwadia Ramadhani, mlowezi wa kizayuni auchoma moto Msahafu Baitul-Muqaddas
Mlowezi mmoja Muisraeli wa kizayuni mwenye misimamo ya chuki ameichoma moto nakala ya Kitabu kitakatifu cha Waislamu, Qur'ani, akiwa katika eneo ambalo halijafahamika katika mji wa Baitul-Muqaddas, siku chache kabla ya kuanza mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Ahmad Tibi, mbunge Mwarabu katika bunge la utawala wa kizayuni wa Israel, Knesset ameandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "mwanaharakati wa kidini Mzayuni kutoka kwenye Wanazi-mamboleo anaichoma moto Qur'ani Tukufu huku uso wake ukiwa wazi".
Tibi amesema, Muisraeli huyo mwenye misimamo ya kufurutu mpaka "hatoadhibiwa kwa sababu yeye ni Myahudi".
Katika video aliyoionyesha yeye Tibi mwenyewe, mlowezi huyo haramu wa Israel anasikika akisema: "Ni nini kinachotokea? Tuko hapa sasa hivi tukisherehekea na kuchoma moto kitabu kitakatifu sana kwa Waislamu, sura baada ya sura, sura zote. Hongera kwetu sisi."
Huku akionekana anauchoma moto Msahafu, mlowezi huyo wa kizayuni anaendelea kusikika akisema: "watu wa Israeli wanaondoa uovu. Hongera kwetu sisi. Ninaitambua vizuri Qur'ani, lakini ni pale tu inapokuwa kama hivi".
Hakuna maoni yaliyotolewa na serikali ya utawala wa kizayuni wa Israel au makundi ya Kiyahudi kuhusu kitendo hicho kiovu, ambacho kimefanywa wakati huu ambapo Waislamu duniani wanaanza kufunga Saumu ya mwezi mtakatifu zaidi katika kalenda ya Kiislamu, wa Ramadhani.../