Salman Al-Farsi; mhangaikaji wa kutafuta haki na ukweli
https://parstoday.ir/sw/news/event-i140692-salman_al_farsi_mhangaikaji_wa_kutafuta_haki_na_ukweli
Assalamu Alaykum mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Tarehe 31 ya mwezi wa nne wa Tir katika kalenda ya Hijria Shamsia ya Kiirani ni siku rasmi katika kalenda hiyo ya Kumuenzi Salman Al-Farsi. Kutokana na tarehe hiyo kusadifiana na Julai 22, makala yetu ya wiki kwa juma hili itaangazia kwa ufupi kisa cha maisha ya sahaba huyo mtukufu aliyeenziwa na kupewa hadhi maalumu na Bwana Mtume SAW. Kuwa pamoja nami basi kuanzia awali hadi tamati ya safari hii.
(last modified 2026-08-15T14:45:24+00:00 )
Aug 15, 2026 13:58 UTC
  • Salman Al -Farsi; Mhangaikaji wia kutafuta haki na ukweli
    Salman Al -Farsi; Mhangaikaji wia kutafuta haki na ukweli

Assalamu Alaykum mpenzi msikilizaji popote pale ulipo. Tarehe 31 ya mwezi wa nne wa Tir katika kalenda ya Hijria Shamsia ya Kiirani ni siku rasmi katika kalenda hiyo ya Kumuenzi Salman Al-Farsi. Kutokana na tarehe hiyo kusadifiana na Julai 22, makala yetu ya wiki kwa juma hili itaangazia kwa ufupi kisa cha maisha ya sahaba huyo mtukufu aliyeenziwa na kupewa hadhi maalumu na Bwana Mtume SAW. Kuwa pamoja nami basi kuanzia awali hadi tamati ya safari hii.

Tunapoidurusu historia ya Uislamu, tunakutana na majina ya shakhsia wengi mashuhuri. Hata hivyo, ni nadra kuwapata watu miongoni mwao ambao walikata masafa kutoka ardhi ya mbali mno na kuweza hatimaye kufika kwenye kitovu cha jamii ya mwanzoni mwa Waislamu kama alivyofanya Salman al-Farsi.Salman alikuwa Muirani ambaye alitumia miaka mingi ya maisha yake, akisafiri kwa madhumuni ya kutafuta na kuijua haki na ukweli. Alizipitia dini na imani tofauti, katika ardhi na maeneo mbalimbali, mpaka hatimaye akafika Madina na kukutana na Bwana Mtume Muhammad SAW, akasilimu na kuupokea Uislamu kwa ujudi wake wote. Salman hakuwa mtu tu miongoni mwa waliokuwa wapya kusilimu wala mmoja tu miongoni mwa masahaba wa Mtume. Kutokana na elimu, imani, uaminifu na shakhsia yake ya kipekee, alikuwa na nafasi na hadhi maalumu miongoni mwa Waislamu mpaka Bwana Mtume Muhammad SAW, akasema kuhusu yeye:“Salman ni katika sisi Ahlul-Bayt.”Kauli hii, ambayo imenukuliwa katika vyanzo na maandiko ya kuaminika ya Kiislamu, inadhihirisha heshima na imani kubwa ambayo Bwana Mtume SAW alikuwa nayo kwa Muirani huyo aliyekuwa na kiu kubwa ya kuijua haki na ukweli.Kisa cha maisha ya Salman si simulizi ya mtu fulani tu. Ni simulizi ya mwanadamu aliyeacha raha, familia na mji wake kwa ajili ya kuutafuta ukweli, na hatimaye akawa mmoja wa shakhsia wenye majina ya kudumu zaidi katika historia ya Uislamu.Salman al-Farsi, ambaye kabla ya kusilimu alikuwa akiitwa Ruzbeh, alizaliwa katika ukoo mmoja mashuhuri nchini Iran, katika eneo ambalo leo hii linahesabiwa kuwa sehemu ya mji wa Esfahan. Baba yake alikuwa mmoja wa watu wakubwa na wanaoheshimika katika jamii, na msimamizi wa moja ya vituo muhimu vya kidini katika zama hizo; na alitamani mwanawe Ruzbeh naye pia aje ashike nafasi yake na kuendeleza njia aliyoishika yeye. Lakini tangu akiwa kijana chipukizi, Ruzbeh alikuwa na akili ya udadisi, ya kuhoji na kutafakari mambo. Hakukubali tu kibubusa kila alichokiona na bila kukichunguza. Alipokuwa akiwaona watu wanakaa na kuomba mbele ya moto, akijiuliza:“Inawezekanaje kitu ambacho mwanadamu yeye mwenyewe ndiye anayekiwasha na kukikoleza, na kinachoweza kuzimwa kwa maji au udongo kidogo tu, kiweze kumkurubisha zaidi kwa Muumba wa ulimwengu?”Masuali hayo yalikuwa cheche ya kuanzia safari ambayo baadaye ilikuja kumfanya mmoja wa watu waliotambulika zaidi katika historia ya Uislamu kutokana na hima yake ya kuhangaika na kutaabika ili kuifikia haki na ukweli. Baada ya tafakuri ya kina, Ruzbeh alifikia hitimisho kwamba ulimwengu hauwezi kuwepo bila ya kuwa na Muumba; na Muumba wa ulimwengu lazima awe juu zaidi ya kila ambacho mwanadamu anaweza kukitengeneza kwa mikono yake. Alisikitishwa na kusononeshwa sana pia na utovu wa usawa na pengo kubwa la kitabaka lililokuwepo kati ya matajiri na maskini. Aliamini kuwa dini isiyomlingania mwanadamu haki, uadilifu na huruma haiwezi kutoa jibu kuhusu hakika na ukweli. Mawazo hayo yalimkosesha raha na utulivu. Ruzbeh alikuwa akiitafuta dini ambayo ingeweza kuikinaisha akili yake na, wakati huohuo, kuupa utulivu moyo wake. Baba yake, ambaye aliona mustakabali wa kidini wa ukoo wake umefungamana na nafsi ya mtoto wake, alijitahidi kuhakikisha anamweka mbali Ruzbeh na mawazo na fikra yoyote mpya.Alimzuia na hata kumwekea mpaka wa wapi pa kwenda na nani wa kuchanganyika naye, ili asije akashawishika na kuathiriwa na fikra zingine. Lakini kiu ya kutaka kuujua ukweli haiwezi kuondolewa kwa pingu za vizuizi. Siku moja, wakati Ruzbeh alipokuwa ametoka nyumbani kwao kwa ajili ya shughuli fulani, alisikia sauti za kundi moja la Wakristo waliokuwa wakifanya ibada, zilizoipa mguso akili yake. Aliingia kanisani na kupitisha masaa mengi kusikiliza na kutazama namna walivyokuwa wakiabudu.Utulivu na unyenyekevu aliouona pale vilikuwa vitu vipya kwake. Mazungumzo yake na mmoja wa viongozi wa dini ya Ukristo yalimfungulia dirisha la mwanga mpya katika maisha yake.Kwa mara ya kwanza, alisikia jina la ardhi ya Sham, ambayo wakati huo ilikuwa miongoni mwa vituo muhimu vya dini hiyo.Kurejea nyumbani kwao Ruzbeh kulikuwa mwanzo wa kuzuka mtafaruku na mvutano mkubwa baina yake na baba yake.Alimtamkia bayana mzazi wake, kwamba aliyoyaona kanisani yalikuwa yamemkurubisha zaidi kwenye ukweli kuliko dini yake ya awali.Kauli hiyo ilikuwa nzito sana kwa baba mtu, ambaye kwa miaka mingi alikuwa akimtayarisha mwanawe kuwa mrithi wake.Alijaribu kutumia kila njia kumbadilisha mawazo mwanawe, lakini ilikuwa kazi bure.Hatimaye, na ili kumzuia asiondoke, alimfungia nyumbani Ruzbeh ili asitoke.Lakini azma ya kijana huyo ya kuutafuta ukweli ilikuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko kizuizi chochote kile.Muda si mrefu baadaye, Ruzbeh alipata habari kwamba kuna msafara unaoondoka kuelekea Sham. Kabla jua halijachomoza, na bila ya mtu yeyote kuwa na habari, Ruzbeh aliondoka nyumbani kwao na katika ardhi alikozaliwa na kujiunga na msafara huo wa safari ambayo haikuwa ya biashara wala ya kwenda kutafuta ulua. Ilikuwa ni safari iliyoanzwa kwa lengo moja tu la kwenda kutafuta hakika na ukweli.Akiwa Sham, alipitisha miaka mingi akiishi kando ya wanazuoni na watawa wa Kikristo. Alijifunza elimu kwa kila mwalimu aliyekutana naye. Na baada ya mwalimu mmoja kufariki dunia, alielekea eneo jingine kutafuta mwalimu mwingine.Safari hiyo ilichukua miaka mingi ya maisha ya Ruzbeh, akisafiri kutoka nchi moja hadi nyingine bila kuvunjika moyo wala kukata tamaa.Hatimaye, mmoja wa walimu wake alimweleza kuwa, wakati wa kudhihiri Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu umekaribia. Alimwambia kwamba, Mtume huyo atadhihiri katika ardhi iliyozungukwa na mashamba ya mitende, na atawalingania watu kumwabudu Mungu Mmoja na wa pekee, kusimamisha uadilifu na kuchunga heshima ya mwanadamu. Ruzbeh aliianza tena safari nyingine.Ilikuwa safari ngumu ambayo hatimaye ilimfikisha katika mji wa Madina uliokuwa ukijulikana zama hizo kama Yathrib.Akiwa huko, na baada ya kukutana na Bwana Mtume Muhammad, rehema na amani za Allah ziwe juu yake na Aali zake, alitambua kwamba, miaka yote ya kuhangaika na kuhimili tabu na mateso ilikuwa imemfikisha kwenye lengo na kituo chake kikuu .Aliukubali kwa mapenzi makubwa Uislamu, na Bwana Mtume SAW akamchagulia jina la Salman. Kuanzia hapo, Salman hakuwa tena Muislamu aliyesilimu karibuni .Alikuwa mmoja wa masahaba wa karibu zaidi wa Bwana Mtume, na akawa miongoni mwa shakhsia mashuhuri zaidi wa zama za mwanzoni mwa Uislamu.Simulizi tutakayosikia katika mwendelezo wa makala hii itathibitisha na kutilia nguvu ukweli huo.

Baada ya muda kupita tangu Waislamu kustakimu na kujipanga katika mji wa Madina, walikabiliwa na moja ya vitisho vikubwa zaidi vya kijeshi vya wakati huo.Muungano mkubwa wa kijeshi wa makabila ya Kiarabu, ukiongozwa na Abu Sufyan, uliandaa jeshi kubwa na kuelekea Madina kwa lengo la kuuangamiza utawala mchanga wa Waislamu. Idadi ya wapiganaji waliokuwa kwenye jeshi hilo la wavamizi ilikuwa kubwa kiasi cha kuwatia hofu na wasiwasi mkubwa watu wa Madina.Bwana Mtume SAW, aliwaita masahaba zake kwa mashauriano ili kufikiria njia za kuilinda Madina. Katika kikao hicho, Salman al-Farsi alitoa pendekezo la mbinu ambayo haikuwa ikijulikana kabla ya hapo miongoni mwa Waarabu.Kwa kutumia tajiriba na uzoefu aliotoka nao kwao Iran, alipendekeza kuchimbwa handaki kandokando ya sehemu za mji zinazoweza kuvamiwa kirahisi, ili kulizuia jeshi la adui lisiweze kuingia mjini Madina.Bwana Mtume SAW alilikubali pendekezo hilo, na Waislamu wote, akiwemo Bwana Mtume mwenyewe, walishiriki katika kazi ya uchimbaji wa handaki.Mbinu na mkakati huo wa kijeshi ulitoa mchango muhimu katika kuvunja njama ya kuuzingira mji wa Madina. Baadaye, tukio hilo likajulikana kama Vita vya Khandaq, vikiwa mojawapo ya matukio muhimu zaidi katika historia ya mwanzoni mwa Uislamu.Wakati wa kushirikiana katika uchimbaji wa khandaqi, kila kundi la Waislamu lilijivunia Salman na kumtaja kuwa ni katika wao.Na hapo ndipo Bwana Mtume Muhammad SAW akatamka kauli iliyobakia milele katika historia ya Uislamu, akiielezea nafasi na hadhi ya Salman kwa kusema: Salmaanu Minna Ahlul-Bayt, yaani“Salman ni katika sisi, Ahlul-Bayt.”Kwa Masahaba wa Bwana Mtume, maneno hayo yalikuwa ishara ya kiwango cha juu kabisa cha heshima na imani ambayo Mtukufu huyo alikuwa nayo kwa Salman.Sahaba huyo, alikuwa mtu aliyefikia nafasi iliyovuka mipaka ya kabila na rangi, kutokana na imani yake, elimu yake, ikhlasi yake na miaka mingi aliyoipitisha kwa lengo la kutafuta hakika na ukweli.

Kuanzia hapo, Salman al-Farsi akawa mmoja wa masahaba mashuhuri zaidi wa Bwana Mtume SAW. Maisha yake yakawa nembo na alama ya uhakika, wa kwamba katika Uislamu, thamani ya mtu haipimwi kwa rangi, lugha au nchi anayotoka, bali hutegemea imani, elimu, maadili na huduma anayoitoa kwa jamii.Kaburi la Salman al-Farsi liko nchini Iraq katika mji wa Mada’in, kusini mashariki mwa mji mkuu Baghdad, ambapo kila mwaka, Waislamu wengi kutoka nchi mbalimbali hulizuru ili kwenda kutoa heshima zao na kuienzi kumbukumbu ya mhangaikaji na mtafutaji huyo mkubwa wa hakika na ukweli.Mpenzi msikilizaji, makala yetu ya wiki kwa juma hili inaishia hapa. Nakushukuru kwa kunisikiliza, na nakuombea kila la kheri, fanaka na baraka maishani…/