WFP: Maeneo yenye Ebola DRC sasa yanakumbwa na njaa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141362-wfp_maeneo_yenye_ebola_drc_sasa_yanakumbwa_na_njaa
Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mapambano dhidi ya mlipuko wa sasa wa Ebola huko  mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu, hayawezi kutenganishwa na juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata chakula cha kutosha.
(last modified 2026-09-11T04:10:54+00:00 )
Sep 11, 2026 04:10 UTC
  • WFP: Maeneo yenye Ebola DRC sasa yanakumbwa na njaa
    WFP: Maeneo yenye Ebola DRC sasa yanakumbwa na njaa

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, mapambano dhidi ya mlipuko wa sasa wa Ebola huko  mashariki mwa taifa hilo la Maziwa Makuu, hayawezi kutenganishwa na juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata chakula cha kutosha.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) nchini DRC, David Stevenson amesema mapigano, watu kuhama makazi na ukosefu wa uhakika wa chakula vinaongeza changamoto katika kukabiliana na Ebola.

Stevenson ameyasema hayo baada ya kutembelea miradi ya WFP katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa nchi.

Stevenson amesema: “Eneo hili limeathiriwa vibaya na mapigano, ukosefu wa uhakika wa chakula na watu kuhama makazi. Hivyo linahitaji mkakati wa kina, unaojumuisha pia msaada wa chakula.”

Akiwa eneo la Kaniola, jimboni Kivu Kusini, Stevenson alitembelea mradi wa lishe unaoungwa mkono na WFP, ambapo alikutana na wanawake wakiwa wamebeba watoto wao pamoja na wananchi wengine wanaonufaika na mpango huo.

Kwa mujibu wa Stevenson, uzoefu wa WFP katika maeneo yenye migogoro unaonesha kuwa watu wenye njaa kali hukabiliwa na changamoto kubwa zaidi wakati wa majanga ya kiafya.

Stevenson anasema hali ya Ituri inaonesha ukubwa wa changamoto inayokabili jamii wakati huo huo ikikabiliana na Ebola, mzozo na kuhama kwa watu kutoka makazi yao.

Hali ya sasa ni kwamba, “kuna zaidi ya watu 500,000 walio katika kiwango cha nne cha IPC cha ukosefu wa uhakika wa chakula. Hapo kumesalia kiwango kimoja tu kufikia vifo vinavyosababishwa na njaa kali.”

Kwa hiyo, anasema, mahitaji ya kibinadamu ni makubwa sana katika eneo ambalo pia linakabiliwa na mlipuko wa Ebola.

Anasema uzoefu unaonesha kues msaada wa chakula unapaswa kuwa sehemu ya mkakati mpana wa kukabiliana na Ebola katika eneo lote lililoathiriwa na hivyo, “lazima kuwe na mpango wa kina unaojumuisha pia msaada wa chakula."

Takwimu rasmi zinaonyesha kuwa, watu 6,686 wameambukizwa Ebola na 3,226 wamefariki dunia DRC tokea ugonjwa huo utangazwe kuibuka nchini humo Katikati ya mwezi Mei. Aidha wagonjwa wengine 819 wanatibiwa au wamewekwa katika wodi za kutengwa.