Israel yaiamuru Uingereza ifunge ubalozi wake mdogo ulioko Baitul Muqaddas Mashariki
Utawala wa kizayuni wa Israel umeutaarifu ubalozi mdogo wa Uingereza ulioko katika eneo la Baitul Muqaddas Mashariki (East Jerusalem) linalokaliwa kwa mabavu, kwamba lazima uwe umeshaufunga ubalozi huo ndani ya muda wa siku 30. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa leo na kituo cha habari cha umma cha Israel KAN.
Uamuzi huo umetangazwa muda mfupi baada ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Ed Miliband kutangaza marufuku ya uagizaji bidhaa zinazotoka kwenye vitongoji haramu vya walowezi wa kizayuni katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu, pamoja na vikwazo vinavyolenga makampuni na watu binafsi wanaohusika katika upanuzi wa vitongoji hivyo.
Kwa mujibu wa KAN, Israel imeupa ubalozi huo wa Uingereza mjini Quds muda wa siku 30 kuhitimisha shughuli zake, na kwamba baada ya hapo wanadiplomasia wa Uingereza walioko huko watapoteza kibali chao cha kidiplomasia.
Akitangaza uamuzi huo ulio dhidi ya maslahi ya kiuchumi ya utawala wa kizayuni jana Jumanne, Miliband alisema serikali ya London itayawekea vikwazo makampuni na watu binafsi wanaosaidia upanuzi wa vitongoji katika Ukingo wa Magharibi.
Katika taarifa ambayo haijawahi kutolewa hapo kabla, Miliband alisema: "Kile ambacho serikali ya Netanyahu inafanya huko Ghaza ni doa kwenye dhamiri ya ulimwengu, na kuna ushahidi unaoongezeka kwamba umefanyika uhalifu wa kivita. Hali huko Palestina ni dharura ya kimaadili. Maangamizi ya kizazi dhidi ya Wapalestina katika sehemu za Ukingo wa Magharibi yanafanywa na "magaidi wa Israel," na serikali ya Israel mara nyingi imekuwa ikifumbia macho suala hili. Na baya zaidi, mawaziri wake wamekuwa wakitoa taarifa na kuchukua hatua za kuunga mkono kuhamishwa kwa nguvu Wapalestina. Hatutabaki bila kujali".
Hayo yanajiri, huku Uingereza, Canada na Ufaransa zikiungana na nchi zingine tisa za Ulaya kutoa taarifa ya pamoja ya marufuku ya kitaifa ya biashara kwa bidhaa zinazotoka kwenye vitongoji haramu vilivyojengwa na utawala wa kizayuni wa Israel katika maeneo ya Palestina ya Ukingo wa Magharibi unayoyakalia kwa mabavu.
Nchi hizo tisa za Ulaya ni Denmark, Uhispania, Finland, Ireland, Iceland, Norway, Poland, Ureno, na Sweden…/