Iran yalaani jinai za utawala wa Kizayuni nchini Lebanon
-
Iran yalaani jinai za utawala wa Kizayuni nchini Lebanon
Jamhuri ya Kiislamuy a Iran imelaani vikali uhalifu na jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni nchini Lebanon, ikisisitiza kupinga mashambulizi na ukiukaji wa haki dhidi ya taifa hilo.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amelaani vikali mashambulizi ya kikatili ya utawala wa Kizayuni katika maeneo mbalimbali nchini Lebanon, yakiwemo Al-Ansar, miinuko ya Ali al-Tahir, Nabatiya al-Fawqa na Deir al-Zahrani.
Mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya watu 11, wakiwemo watoto watatu na wanawake wawili kutoka familia moja, huku watu wengine kadhaa wakijeruhiwa. Aidha, mashambulizi hayo yamesababisha uharibifu wa maeneo ya makazi na majengo ya kiraia.
Esmail Baghaei, akizungumza Jumamosi usiku, amelaani pia ukimya na kutokuchukua hatua Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Amesisitiza haja ya kusitishwa mara moja vitendo vya uchokozi vya utawala dhalimu wa Israel kusini mwa Lebanon na kuondoka mara moja katika maeneo ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Aidha, msemaji huyo amepongeza muqawanma wa heshima wa wananchi wa Lebanon dhidi ya uchokozi wa utawala unaokalia maeneo yao, akisisitiza kuwa Lebanon ina haki ya kisheria na halali kutumia njia zote za kujilinda dhidi ya uchokozi huo.
Baghaei amesisitiza pia mshikamano wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Lebanon katika juhudi za kulinda mamlaka ya kitaifa, uhuru na heshima ya nchi hiyo.