Mauaji ya Kimbari: Sera Rasmi ya Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140710-mauaji_ya_kimbari_sera_rasmi_ya_wazayuni
"Mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi ni mradi rasmi wa utawala wa Israel." Kwa maneno haya, Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ameangazia uhalisia wa kisiasa na kisheria katika ardhi hizo.
(last modified 2026-08-16T05:18:10+00:00 )
Aug 16, 2026 05:10 UTC
  • Mauaji ya Kimbari: Sera Rasmi ya Wazayuni

"Mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi ni mradi rasmi wa utawala wa Israel." Kwa maneno haya, Francesca Albanese, Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya haki za binadamu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, ameangazia uhalisia wa kisiasa na kisheria katika ardhi hizo.

Kwa mtazamo wa Albanese, suala la Palestina si suala la vita tu, operesheni chache za kijeshi, au ukiukwaji wa haki za binadamu unaotokea mara kwa mara katika ardhi hizo, bali ni mfumo ambapo uvamizi, ubaguzi, ukandamizaji, mateso, kufukuzwa makazi, na mauaji, yote hayo yanatumikia mradi mmoja. Ifuatayo ndiyo sehemu iliyo wazi zaidi ya msimamo wa Ripota Maalum wa Umoja wa Mataifa: "Mauaji ya kimbari na ubaguzi wa rangi haviwezi kuchukuliwa kama madhara ya pembeni tu ya vita; kwa tathmini yake, ni sehemu muhimu ya mradi mzima wa utawala wa Kizayuni."

Katika ripoti zake, Albanese amejitahidi kuyaondoa matukio yanayoendelea huko Palestina katika muktadha finyu wa "mgogoro kati ya Israel na Hamas." Kwa mtazamo wake, Gaza haiwezi kueleweka bila kuzingatia miongo kadhaa ya uvamizi, mzingiro, upanuzi wa vitongoji vya walowezi, ukimbizi na kupokonywa haki za Wapalestina. Kwa mtazamo huu, vita vilivyofuatia matukio ya Oktoba 7 2023 haviashirii mwanzo wa mgogoro huo, bali ni hatua mpya katika mgogoro wa muda mrefu kihistoria. Ripoti ya Albanese ya Machi 2026 kuhusu mateso dhidi ya Wapalestina inafuata mantiki hiyo hiyo. Kukamatwa kwa umati watu wasio na hatia, mateso, unyanyasaji wa kijinsia, udhalilishaji, njaa, na mazingira ya kikatili gerezani, sambamba na mashambulizi ya mabomu, mzingiro, na kufukuzwa katika makazi kwa nguvu, si matukio yasiyohusiana. Francesca Albanese anayaona kama vipengele vya mfumo uliopangwa barabara, na unaovuka mipaka ya vitendo vya watu binafsi na kufikia kiwango cha muundo wa sera za serikali. Hapa ndipo maana ya "uwajibikaji" inapobadilika ghafla. Ikiwa uhalifu ni matokeo ya makosa ya askari wachache tu, basi ni hao askari pekee ndio wanapaswa kufikishwa mahakamani. Hata hivyo, ikiwa vurugu hizo zinatokana na sera za umma, uwajibikaji hauwezi kuishia kwa mtu wa ngazi ya chini kabisa katika mnyororo huo. Mifumo ya kamandi, maamuzi ya kisiasa, usambazaji wa silaha, uungwaji mkono wa kidiplomasia, na hata mahusiano ya kiuchumi, yote haya yanapasa kuchunguzwa kwa kina: nani anabeba gharama ya kuendeleza hali hii, na nani ananufaika nayo? Ni katika muktadha huu ndipo Albanese anasema: "Hakuna 'Israel nzuri' na 'Israel mbaya'; yote ni Israel." Kabla ya kauli hii kumlenga mkazi mmoja mmoja wa Israel, inalenga mfumo wa mamlaka ambao, kwa mtazamo wake, umebadilisha hali ya uvamizi na ubaguzi kutoka kuwa jambo la muda mfupi na kuwa uhalisia wa kudumu.

Sera inapoendelea kwa miaka mingi, ikatekelezwa na taasisi za serikali, ikafuatiliwa na jeshi, na kuungwa mkono kwa rasilimali za umma, uwajibikaji hauwezi tena kuhusishwa na "watu wachache wabaya" tu.

Hapa ndipo ukimya wa Magharibi wenyewe unakuwa suala tata. Mataifa ya Magharibi mara nyingi yamechukulia vikwazo, mashinikizo ya kiuchumi, vikwazo vya silaha, na kutengwa kidiplomasia kama zana halali za sera za kigeni katika kukabiliana na ukiukwaji wa haki za binadamu duniani. Hata hivyo, suala hili linapouhusu utawala wa Kizayuni, lugha ya siasa hubadilika ghafla: Usalama hubadilika kuwa sheria ya kimataifa, "kujilinda" huwa ngao dhidi ya uwajibikaji, ambapo wakosoaji badala ya kupewa majibu yanayotegemea ushahidi, hukabiliwa na shutuma za kucheza mchezo wa kisiasa. Mkanganyiko huu ndio chanzo cha mgogoro wa itibari wa Magharibi.

Uadui wa Israel na baadhi ya serikali za Magharibi dhidi ya Albanese hasa unapasa kueleweka katika muktadha huu. Ametuhumiwa kufanya upendeleo na kuwa na chuki dhidi ya Mayahudi, ambapo hata kumekuwa na majaribio kadhaa ya kumwondoa katika wadhifa wake. Ni wazi kuwa, jibu la ripoti hiyo ya haki za binadamu haliwezi kuwa ni kushambuliwa mwandishi wake. Ikiwa ushahidi una kasoro, unapaswa kupingwa kwa hoja; ikiwa takwimu si sahihi, ni lazima zirekebishwe kwa kuwasilisha nyaraka sahihi; ikiwa ushahidi wa mashuhuda hauna mashiko, sababu zake zinapaswa kuwekwa wazi. Kunyamazisha mkosoaji si jibu kwa uhalifu. Hapa ndipo suala la Palestina linapovuka mipaka ya mzozo wa kikanda na kuwa mtihani mkubwa kwa mfumo wa kimataifa.

Albanese ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuutenga utawala wa Kizayuni, kusitisha biashara inayohusiana na uvamizi na kuacha kuuzia silaha. Madai haya yanaweza kukabiliwa na upinzani wa kisiasa, lakini swali la msingi lililojificha nyuma yake haliwezi kupuuzwa nalo ni kuwa je, ikiwa sheria za kimataifa zinahusu mataifa yote kwa usawa, kwa nini basi utawala mmoja ufanyiwe upendeleo na kuepushwa na kanuni zilezile zinazoyabana mataifa mengine? Kwa kubainisha kuwa "Nakba haijawahi kwisha," Ripota huyo Maalumu wa Umoja wa Mataifa anagusia jeraha ambalo halijawahi kupona katika kumbukumbu za Wapalestina. Kwa Wapalestina, Nakba sio tukio la kihistoria pekee; ni mfululizo endelevu wa kuhamishwa kwa lazima, uvamizi, kunyimwa haki na vita. Katika muktadha huu, Gaza ya leo inawakilisha kiini cha mzozo katika historia ndefu, na si mwanzo wake. Jinai zilizofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita ni za wazi na zisizofichika kiasi kwamba haziachi shaka yoyote kuhusu asili ya ubaguzi wa rangi na mfumo wa 'apartheid' unaoendelea katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala ghasibu wa Israel. Vitendo hivi vya kikatili vimekuwa mtihani mkubwa kwa serikali za Magharibi zinazodai kuheshimu maadili ya kibinadamu, mtihani ambao bila shaka nchi za Magharibi tayari zimeufeli. Ni wazi kuwa ushawishi wa kimaadili na itibari ya serikali za Magharibi vimeporomoka kutokana na msimamo wao wa kutochukua hatua, bali hata uungaji mkono wao wa wazi wazi kwa jinai za kutisha za utawala wa Kizayuni.