Baghaei: Iran haibadili sera zake kwa kushinikizwa na kuainishiwa muda
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i140746-baghaei_iran_haibadili_sera_zake_kwa_kushinikizwa_na_kuainishiwa_muda
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haibadilishi sera zake kutokana na shinikizo au muda wa mwisho uliowekwa.
(last modified 2026-08-17T12:37:41+00:00 )
Aug 17, 2026 12:36 UTC
  • Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran
    Esmail Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haibadilishi sera zake kutokana na shinikizo au muda wa mwisho uliowekwa.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Jumatatu kuhusu madai ya kumalizika muda wa mwisho wa siku 60 unaohusishwa na makubaliano ya Islamabad, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, alisema: "Kwanza kabisa, jambo kama hilo halipo. Hakuna kutajwa muda wa mwisho wa siku 60 katika maandishi ya makubaliano hayo. Iran si nchi inayounda sera zake kwa msingi wa shinikizo au mipaka ya muda; tunafanya maamuzi kulingana na maslahi yetu ya kitaifa na tathmini zetu wenyewe."

"Hatukuanzisha mazungumzo yoyote hata kidogo, na Marekani ilikiuka makubaliano hayo tangu mwanzo; kwa hivyo, suala la muda wa siku 60 halina umuhimu wowote," alisema Baqaei.

Aidha amesisitiza kuwa Iran itaamua hatua zake kulingana na maslahi ya taifa na tathmini yake yenyewe ya hali inayoendelea, badala ya kufuata muda wa mwisho uliowekwa na wahusika wa nje.

Msemaji huyo pia alisema kuwa vikosi vya jeshi la Iran vinafuatilia kwa karibu hali inayoendelea katika eneo hilo. "Vikosi vyetu vya jeshi vinafuatilia kwa makini kila hatua au harakati," alisema, huku akiongeza kuwa Tehran inaendelea na juhudi za kuimarisha uhusiano na nchi za eneo.

Akijibu madai ya Marekani kwamba Washington ilikuwa imebadilisha vipaumbele vyake kuhusiana na Iran, Baqaei alisema kuwa maelezo yanayobadilika-badilika yanaashiria kuendelea mkanganyiko, na akasisitiza kuwa vita dhidi ya Iran vilianzishwa bila msingi halali.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya Nje ya Iran amesema pia kuwa, awali Washington ilihalalisha operesheni hiyo ya kijeshi kwa kutaja tishio la karibu kutoka Iran, lakini baadaye Pentagon ilikanusha kuwepo kwa tishio la namna hiyo.