Russia yaonya shambulizi dhidi ya Iran linaweza kuwasha moto wa kikanda
-
Balozi wa Russia mjini Tehran Alexey Dedov
Balozi wa Russia mjini Tehran amezikosoa vikali Marekani na Israel kwa kufuata “sera za uharibifu,” akionya kuwa uchokozi wowote dhidi ya Iran unaweza kusababisha “athari zisizotabirika na zenye maangamizi makubwa” katika eneo la Asia Magharibi na kwingineko duniani.
Alexey Dedov ameiambia televisheni ya RT kwamba, “kwa bahati mbaya, sera za uharibifu za Marekani, Israel, na baadhi ya nchi za Magharibi zimesababisha kuongezeka kwa kiwango kikubwa kwa mivutano eneo la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi) katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.”
Mwanadiplomasia huyo wa Russia ameongeza kuwa, “tishio kubwa zaidi ni hatari ya kuongezeka kwa mapigano ya kijeshi katika eneo hilo, hali inayobeba hatari kubwa inayozidi mipaka ya Mashariki ya Kati.”
Amesema kuwa, katikati ya wito “usio na uwajibikaji” kutoka katika miji mikuu ya Magharibi unaosukuma kuelekea uchokozi mpya dhidi ya Iran, kwa visingizio vinavyoanzia madai ya kuunga mkono waandamanaji hadi juhudi za kuivunja programu ya makombora ya kujihami ya Iran, Moscow “inakataa kikamilifu aina hii ya kuingilia mambo ya ndani ya Iran kwa njia ya kuhujumu, jambo linalokiuka misingi ya uhuru wa mataifa na mipaka ya kitaifa.”
Dedov amesisitiza kuwa Russia iko tayari kuchangia katika suluhu ya kidiplomasia ya hali ya sasa katika eneo hilo.
Akizungumzia mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanayoendelea kati ya Tehran na Washington, amesema: “Tunafuatilia kwa karibu hali hiyo na, endapo tutaombwa, tuko tayari kutoa msaada.”
Mjumbe huyo alibainisha kuwa, “wanadiplomasia wa Iran daima wako tayari kushirikiana na mara kwa mara huweka mbele mbinu za kisiasa na kidiplomasia katika jukwaa la kimataifa, jambo linalotofautisha kazi yao chanya na matamshi ya uchokozi na yasiyo na msingi ya wahusika wa Magharibi.”
Amesema kuwa “mgogoro wa kidiplomasia kati ya Iran na Magharibi” unatokana na “nia ya kulazimisha Iran kujisalimisha kwa mifumo ya kinyonyaji ya kikoloni-mamboleo ya Marekani na Umoja wa Ulaya.” Aidha amesema vikwazo vingi haramu, kuingilia mambo ya ndani ya Iran, hatua za kulazimisha, na shinikizo la kijeshi na kisiasa ni miongoni mwa zana zinazopendelewa na Magharibi kufikia lengo hilo.
Dedov amesema Russia inatumaini diplomasia itashinda, akionya kuwa vita dhidi ya Iran vitasababisha huzuni na vifo pekee, havitatatua chochote, na vinaweza kulivuta eneo zima la Asia Magharibi katika mgogoro wa machafuko usiodhibitika.