Kwa nini Marekani imeshindwa na Iran
https://parstoday.ir/sw/news/event-i140596-kwa_nini_marekani_imeshindwa_na_iran
Hujambo mpenzi msikiilizaji. Je, matukio nyeti katika kanda ya Asia ya Magharibi yanaweza kueleweka vyema zaidi kwa mtazamo wa mwanadiplomasia wa Kijapani? Katika kipindi hiki, tunatupia jicho kitabu kilichopewa jina "Why America Was Defeated by Iran" (Kwa Nini Marekani Imeshindwa na Iran) kilichoandikwa na Mitsugu Saito, balozi wa zamani wa Japan nchini Iran.
(last modified 2026-08-11T11:44:25+00:00 )
Aug 11, 2026 11:38 UTC
  • Mitsugu Saito, afafanua kwa nini Marekani imeshindwa na Iran
    Mitsugu Saito, afafanua kwa nini Marekani imeshindwa na Iran

Hujambo mpenzi msikiilizaji. Je, matukio nyeti katika kanda ya Asia ya Magharibi yanaweza kueleweka vyema zaidi kwa mtazamo wa mwanadiplomasia wa Kijapani? Katika kipindi hiki, tunatupia jicho kitabu kilichopewa jina "Why America Was Defeated by Iran" (Kwa Nini Marekani Imeshindwa na Iran) kilichoandikwa na Mitsugu Saito, balozi wa zamani wa Japan nchini Iran.

Ni kitabu hiki ambacho kwa kuzingatia uzoefu wa mwandishi wake wa miongo minne katika eneo la Asia Magharibi, kinatoa mtazamo tofauti kuhusu nafasi ya kimkakati ya Iran, umuhimu wa Lango Bahari la Hormuz, pamoja na uchambuzi wake kuhusu makablliano kati ya Iran na Marekani. 

Wakati mwingine, ili kuielewa nchi, kusoma simulizi ya mtu aliyeishi miongoni mwa watu wake kwa miaka mingi kunatoa picha ya wazi zaidi kuliko ripoti nyingi za kisiasa au za vyombo vya habari hasa ikiwa msimulizi ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu mkubwa ambaye ameshuhudia matukio ya kikanda kwa karibu na moja kwa moja, na si kwa kuketi ofisini tu.

Makala yetu ya wiki hii,  kama tulivyotangulia kusema, inatupia jicho kitabu Why America Was Defeated by Iran kilichoandikwa na Mitsugu Saito, balozi wa zamani wa Japan nchini Iran. Saito ni mwanadiplomasia aliyefanya kazi katika eneo la Asia ya Magharibi kwa zaidi ya miongo minne na uzoefu wake wa kuhudumu jijini Tehran na Tel Aviv umemfanya kuwa na mtazamo wa kipeee na wa kupewa nazingatio kuhusu masuala ya eneo la Asia Magharibi. 

Katika kitabu chake hicho, Saito amejaribu kujibu maswali kwamba kwa nini katika makabiliano ya karibuni kati ya Iran na Marekani  kile kilichojiri uwanjani kimekuwa tofauti na utabiri mwingi? 

Kabla ya kuzama katika masuala ya kisiasa na kijeshi, anaanzia kwenye nukta anayoiamini kuwa ndiyo ufunguo wa kuelewa mlingano mzima wa masuala ya eneo hilo yaani: Lango-Bahari la Hormuz.

Lango-Bahari wa Hormuz ni njia muhimu ya baharini iliyoko kusini mwa Iran, ambayo tangu zama za kale imekuwa lango muhimu la mawasiliano ya baharini na biashara za kimataifa. Njia hiyo ya majini sio tu inatambulika kuwa kiungo cha mawasiliano na biashara, lakini inajulikana pia kama alama na nembo ya umuhimu wa kijiografia na kihistoria ya Iran.

Kwa mtazamo wa mwandishi huyo, Lango-Bahari la Hormuz sio tui njia nyembamba ya maji  kati ya Iran na Oman, bali ni njia kuu ya kimataifa ya usafirishaji wa nishati na mshipa muhimu wa uhai kwa uchumi wa mataifa mengi. Kwa sababu hiyo, Saito anaamini kuwa bila kuelewa nafasi ya kimkakati ya Iran na dhima ya Lango la Hormuz, haiwezekani kuelewa vyema matukio ya Ghuba ya Uajemi au kuchambua uhusiano tata kati ya Iran na Marekani. Nuta hiyo ni mwanzo wa simulizi yake katika kitabu "Why America Was Defeated by Iran". 

Mitsugu Saito anaanza simulizi yake si kutoka katika uwanja wa vita, bali katika jiografia; kuanzia katika Lango Bahari la Hormuz ambao kwenye ramani linaweza kuonekana kama njia nyembamba tu ya majini, lakini kiuhalisia, ni mojawapo ya maeneo muhimu zaidi duniani.

Anaandika kuwa, sehemu kubwa ya mafuta yanayoingizwa nchini Japan na katika mataifa mengine mengi kutoka Asia Magharibi lazima yapite kwenye Lango-Bahari la Hormuz ili kufika Bahari ya Hindi; ni njia ya majini yenye upana wa kilomita thelathini na tatu tu katika nukta nyembamba zaidi, na katika baadhi ya njia za usafiri wa meli;  meli kubwa sana za kubeba mafuta hulazimika kupita kwenye njia zenye upana wa kilomita chache tu. Kwa sababu hiyo, kwa mtazamo wa mwandishi, anasema mgogoro wowote katika eneo hilo si suala la usalama kwa ajili ya Asia ya Magharibi pekee, bali pia unaathiri moja kwa moja uchumi wa nchi kama vile Japan na nyinginezo.

Saito amefikia hitimisho ambalo huenda ndilo msingi muhimu zaidi wa kitabu chake. Anaamini kuwa nchi inayodhibiti pwani ya kaskazini ya Lango-Bahari la Hormuz si mchezaji na mshiriki wa kikanda tu, bali ni nguzo muhimu inayoathiri usalama wa nishati duniani. Kwa sababu hiyo, kwa mtazamo wake anasema: Kuielewa Iran si muhimu tu kwa majirani zake, bali pia ni dharura ya kimkakati kwa nchi zilizo umbali wa maelfu ya kilomita.

Ili kusisitiza hoja hii, mwandishi anaashiria uzoefu wake binafsi. Anaeleza kuwa, katika kipindi cha miongo minne ya kazi yake ya kidiplomasia alihudumu katika nchi saba za Asia Magharibi, na ni miongoni mwa  wanadiplomasia wachache waliowahi kuhudumu nchini Iran na huko Israel; uzoefu ambao, kwa maneno yake mwenyewe, umemuwezesha kulinganisha mazingira matatu tofauti: Iran, Ulimwengu wa Kiarabu na Israel. Uzoefu huo ndio msingi wa sehemu kubwa ya uchambuzi wake katika kitabu hicho. Kisha anaashiria kitabu kingine alichochapisha miaka michache iliyopita ambacho ndani yake alitadharisha kuwa utegemezi mkubwa wa Japan kwa mafuta kutoka Ghuba ya Uajemi ungeweza kuiweka nchi hiyo katika hatari iwapo kungetokea mgogoro wowote katika Lango-Bahari la Hormuz. Kwa mtazamo wake, indhari hiyo imekuwa na umuhimu mkubwa hii leo kuliko huko nyuma; kwa sababau ukwamishaji wowote wa kuvuka meli za mafuta katika eneo hilo haungeathiri tu bei ya mafuta, bali pia ungesababisha mlolongo wa athari mbaya za kiuchumi duniani kote.Kwa msingi huo, Mitsugu Saito anaamini kuwa uhusiano kati ya Iran na Japan si wa kidiplomasia au kiuchumi pekee; bali ni sehemu ya mlinganyo wa usalama wa nishati katika Asia ya Mashariki. Anaenda mbali zaidi na kuandika: Ustawi wa kiuchumi wa Japan na mataifa mengine yanayotegemea mafuta ya Asia Magharibi unategemea kwa kiasi kikubwa utulivu na amani katika Ghuba ya Uajemi na kudumisha uhusiano wenye tija na Iran; uchambuzi unaoonyesha kuwa mwandishi anaihesabu Iran si tu mzalishaji wa mafuta, bali pia upande muhimu katika mlingano wa kijiopolitiki duniani. Hata hivyo utangulizi huu ni msingi tu kwa wa kuingi katika mjadala mkuu wa kitabu —ambapo mwandishi anajaribu kueleza kwa nini katika vita vya karibuni kati ya Iran na Marekani pande mbili hizo zimeingia vitani zikiwa na mitazamo na mantiki tofauti kikamilifu; tofauti ambazo, kwa mtazamo wake, zilichangia pakubwa katika mwenendo wa matukio na matokeo ya mzozo huo.

Baada ya kuelezea umuhimu wa kimkakati wa Lango-Bahari La Hormuz kama msingi wa uchambuzi wake, mwandishi anaingia katika mojawapo ya sehemu zenye mvuto mkubwa zaidi katika kitabu chake — sura ambayo kichwa chake kinaakisi vyema mtazamo wake: Trump wa "poker" dhidi ya Iran ya "chess."

Mitsugu Saito anaamini kuwa ili kuelewa mzozo kati ya Iran na Marekani haitoshi kulinganisha uwezo wa kijeshi wa nchi mbili hizo, bali pia kuna ulazima kuelewa jinsi pande zote mbili zinavyofikiria na kufanya maamuzi. Mitsugu anaamini kuwa, Marekani na Iran katika vita hivyo ilikuwa zinacheza michezo miwili tofauti kabisa; yaani upande mmoja unafuata kanuni za Poker, na mwingine unafuata kanuni za Chess.

Anasema, Donald Trump ana mienendo inayoshabiana na ya mchezaji wa Poker katika sera zake za nje; ni mchezaji anayekuza mambo, anayetumia mbinu za kushtukiza na kuwaslisha matwaka ya kuzidi kiwango ili kuvuruga mahesabu ya upande wa pili, huku lengo kuu likiwa ni kufikia makubaliano yenye maslahi mapana katika meza ya mazungumzo. Anaiona mbinu hii kama aina ya "hila ya kisiasa" ambayo katika utamaduni wa kisiasa wa Marekani, hasa katika lugha ya biashara ya Trump  Trump, ina rekodi inayofahamika. 

Saito anamini kuwa upande wa Iran unaichambua tabia hii kwa mtazamo tofauti. Anaandika kwamba, kinyume na mantiki ya poker, watunga sera wa Iran kwa kawaida huchambua maamuzi ya upande mwingine kulingana na uhalisia, si mbinu za hila. Kwa sababu hiyo, wanapokabiliwa na tishio au matakwa makubwa kupita kiasi, hawalitambui jambo hilo kama mbinu ya kisaikolojia pekee; badala yake, hutayarisha jibu mwafaka na madhubuti dhidi ya hatua hiyo. Mwandishi anafananisha mbinu hii na mtazamo unaotegemea kanuni ya "majibizo" (reciprocity); kwa maana kwamba, kila kitendo hukabiliwa na jibu linalolingana nacho au sawia. 

Kwa mtazamo wake, tofauti hiyo katika namna ya kufikiri imekuwa sababu ya pande zote mbili kushindwa kuelewa kwa usahihi nia halisi ya kila upande. Pale upande mmoja ulipoona kuongezeka mashinikizo kama njia ya kupata nguvu ya ziada katika mazungumzo, upande wa pia uliyaona mashinikizo hayo hayo kama ishara ya kuanza kwa awamu mpya ya makabiliano. Kwa mtazamo wa mwandishi, sehemu kubwa ya kutoelewana na kushtadi mivutano imetokana na tofauti hiyo ya kimtazamo.

Hata hivyo, uchambuzi wa Saito hauishii hapa. Anaamini kuwa, tofauti kati ya Iran na Marekani haikuwa tu kuhusu utaratibu wa mazungumzo, bali pia zimedhihiri katika namna ya kuutazama muda.

Kwa mujibu wa maandiko yake anasema Trump alitaka matokeo ya haraka kama mchezaji anayetaka kuainisha matokeo ya mechi kwa muda mfupi kadiri inavyowezekana. Kinyume chake, Iran imetaka kurefusha mchezo, ikiamini kuwa vita vya kumomonyoana vingeipa fursa zaidi ya kubadili mlingano wa nguvu.

Ili kuelezea tofauti hii, mwandishi Mitsugu Saito anatumia mfano mwingine wa kuvutia. Anaandika kuwa, Trump ni kama mwanariadha wa mbio fupi; ni mwanasiasa anayefadhilisha kuhitimisha mambo ndani ya siku au wiki chache na kuhamia kwenye ksi inayofuata haraka sana. Lakini Iran kwa mtazamo wa Saito, imejitayarisha kwa mbio ndefu; mashindano ambayo yamejikita katika subira, ustahimilivu na kudhoofisha nguvu ya adui, hatua kwa hatua.

Kwa mtazamo wa Mitsugu Saito, tofauti kuu kati ya Iran na Marekani haikuwa tu katika aina ya mtazamo wa kisiasa au mtindo wa mazungumzo; pia imedhihirika katika kuchagua mkakati wa kijeshi. Anasema kwamba tangu mwanzo, Iran haikuingia katika ushindani ambao matokeo yake yaneainishwa na ubora wa kiteknolojia na nguvu ya Marekani na Israel. Badala yake, ilichagua mkakati unaojulikana katika fasihi ya kijeshi kama vita visivyo na ulinganifu, (asymmetric warfare), mkakati unaolenga udhaifu wa mpinzani badala ya mapambano ya moja kwa moja.

Mwandishi anaelezea kwamba, Iran ilikuwa inajua vyema kwamba mifumo ya ulinzi ya anga ya Marekani na Israel, ingawa ni ya kisasa sana, lakini ina gharama kubwa za kuitunza na kuiendesha. Kwa upande mwingine, kutengeneza makombora ya kujikinga na mombora na kuzalisha mbadala wake pia kunachukua muda mrefu. Wakati huo huo utumiaji wa ndege zisizo na rubani na makombora ya bei nafuu unaweza kumlazimisha adui kutumia vifaa na zana zake za gharama kubwa sana kukabiliana na kila shambulio. Kwa msingi huo, Saito anaamini kwamba tofauti hii ya gharama, polepole imekuwa mojawapo ya mambo muhimu zaidi katika kubadili mlingano wa nguvu.

Anaamini kwamba Iran imefanya jitihada za kupanua medani ya vita kutoka kwenye uwanja wa kijeshi hadi uwanja wa uchumi na nishati. Anaandika kwamba wakati wowote usalama wa Lango-Bahari la Hormuz unapotishiwa, athari zake za kwanza huwa ni kuongeza bei ya kimataifa ya mafuta; Tukio ambalo huathiri haraka bei ya mafuta, usafirishaji, bima na bidhaa nyingi. Kwa mtazamo wa mwandishi, katika nchi kama Marekani ambako sehemu kubwa ya maisha ya kila siku ya watu inategemea utumiaji wa magari, ongezeko la bei ya petroli si suala la kiuchumi tu; Badala yake, linaweza kuwa suala la kisiasa na kuifanya serikali ikabiliwe na mashinikizo ya maoni ya umma.

Mwandishi wa kitabu "Why America Was Defeated by Iran" anaamini kwamba, hii ndiyo sababu ya mzozo kati ya Iran na Marekani kugeuka kutoka makabaliano ya kijeshi hadi vita vya muda, uchumi na nishati; vita ambavyo, kadri mapigano yanavyochukua muda mrefu zaidi, ndivyo mashinikizo kwa Marekani yanavyochukua sura mpya. Mwandishi anaamini kwamba mabadiliko haya katika uwanja wa vita ni sehemu ya mkakati wa Iran wa kugeuza vita vya kijeshi kuwa vita vya kuachosha na kummomonyoa adui.