Gabon yapiga marufuku matumizi ya mitandao ya kijamii, yasema inachochea migawanyiko
Serikali ya Gabon imepiga marufuku kwa muda matumizi ya mitandao ya kijamii, ikisema kuwa inahusika na kuchochea migogoro na migawanyiko ndani ya jamii.
Msemaji wa Mamlaka ya Mawasiliano ya Gabon, Jean-Claude Mendome amesema, mitandao hiyo imekuwa ikihusika kwa kiasi kikubwa na usambaaji wa taarifa potofu, mmomonyoko wa maadili na kutishia usalama wa taifa hilo.
Mendome ameongeza kuwa “maudhui zisizofaa, za kashfa, chuki na matusi” zinadhoofisha heshima ya mtu, maadili ya umma, mshikamano wa kijamii, uthabiti wa taasisi za Jamhuri na usalama wa taifa.
Pamoja na hayo, msemaji huyo wa Mamlaka ya Mawasiliano ya ya serikali ya Libreville amebainisha kuwa, "uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na uhuru wa maoni na ukosoaji," unabaki kuwa "haki ya kimsingi iliyowekwa nchini Gabon".
Chini ya mwaka mmoja baada ya kuchaguliwa, Rais wa Gabon Brice Oligui Nguema amekabiliwa na wimbi la kwanza la machafuko ya kijamii, huku walimu na watumishi wengine wa umma wakitishia kugoma.../