Lavrov: Wanajeshi wa Ukraine Wanahusika na Ugaidi dhidi ya Nchi za Afrika
-
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov
Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, Sergey Lavrov, amesema kuwa Moscow imetiwa wasiwasi na ripoti zinazoashiria kuwa wanajeshi wa Ukraine wanahusika katika operesheni zinazotekelezwa na makundi haramu ya wanamgambo dhidi ya nchi za ukanda wa Sahel barani Afrika.
Akizungumza baada ya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana, Samuel Okudzeto Ablakwa, siku ya Jumatatu, Lavrov amesisitiza kuwa kuhusika kwa wanajeshi waliopo kazini, badala ya mamluki binafsi, ni ishara ya wazi kwamba hatua hizo zinafanywa katika ngazi ya kiserikali.
Waziri huyo wa Russia pia amewalaumu wakoloni wa zamani kwa kuchochea ugaidi barani Afrika. Amesema: “Si siri kwamba jambo hili linafanywa na Ufaransa, ambayo inashirikiana moja kwa moja na makundi haramu ya wanamgambo, inawapa silaha, inawafadhili, na inawapa maelekezo.”
Lavrov amesisitiza kuwa: “Awali ya yote, [Ufaransa] inawapa maagizo ya kuleta matatizo kwa nchi hizo, katika kesi hii, ukanda wa Sahara-Sahel, ambazo zimeamua hatimaye, kabisa na bila kurejea nyuma, kukata uhusiano na wakoloni wao wa zamani na zinafuata mkondo huu kwa msimamo thabiti.”
Nchi za Sahel zimekuwa zikipambana na uasi wa magaidi wa Kitakfiri tangu mwaka 2012.
Mwaka 2023, Mali, Burkina Faso, na Niger, mataifa matatu yanayoongozwa na maafisa wa kijeshi ambayo yalikuwa makoloni ya Ufaransa, yaliunda Muungano wa Mataifa ya Sahel (AES) baada ya kusitisha ushirikiano wa ulinzi na Ufaransa. Nchi hizo tatu zinaishutumu Ufaransa kwa kushindwa kudhibiti uasi huo. Tangu wakati huo, mataifa haya matatu yameimarisha ushirikiano na Russia.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ghana amesema kuwa eneo la Sahel ni “kitovu cha ugaidi na itikadi kali za vurugu duniani.” Amesema kuwa Ghana na Russia zimekubaliana kushirikiana ili kusaidia Niger, Burkina Faso, na Mali katika kushughulikia changamoto za kiusalama zinazolikabili eneo hilo.
Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ghana pia ameishukuru Russia kwa kuunga mkono azimio la Umoja wa Mataifa lililotangaza biashara ya utumwa ya kuvuka Atlantiki kuwa uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu. Ablakwa amesema: “Tunaitazama Russia kama mshirika anayeaminika.”